
Msanii maarufu wa Singeli, Dulla Makabila ameibuka na kumwangukia miguuni Supastaa wea Bongo Fleva na CEO wa Lebo ya WCB, Diamond Platnumz akimuomba amsamehe kutokana na yaliyotokea hapo nyuma ili arejee tena kuwa mwanafamilia wa Wasafi.
Makabila amesema kilichotokea ilikuwa ni kuyumbishwa na watu wake wa pembeni na kumuona Diamond hafai jambo ambalo limemfanya kukosa vitu vingi kwenye career yake ya muziki.
“Diamond Platnumz bigi ni ukweli usiopingika kwamba nimepoteza mtu muhimu sana kwenye career yangu ambaye ni wewe na vita pekee ya kuomba radhi haiendewi na silaha.
“Mikono yangu ipo nyuma naomba unisamehe sana kaka kwa yote yaliyotokea nikisema leo nisielezee hisia zangu na jinsi navyojisikia baada ya kuwa mbali na wewe na familia nzima ya Wasafi kisa eti labda nitaonekana najishusha au nina shobo au sijiamini na kipaji changu nitakuwa najidanganya mwenyewe.

“Maana ni ukweli usiopingika kwamba Dulla Makabila alikuwa staa kabla ya kuwa na Wasafi na ni ukweli usiopingika kwamba WASAFI ndio walifanya Dulla Makabila awe brand na kutofautiana na wasanii wenzake wa singeli.
“Naweza nisiwe sehemu ya historia ya mafanikio yako ila naamini wewe una nafasi kubwa kwenye maisha yangu. Sihitaji kuelezea ni mangapi mazuri uliyafanya kwangu maana yananitafuta ndani kwa ndani.
“Wala sitaki kumlaumu mtu wala kusema fulani ndio kaniponza ila uongo hautaenda mbali kama ukweli kuwa kuna mahali nimeteleza, ninahitaji kusamehewa. Bigi naiomba nafasi hii tena ya kuwa miongoni mwa wale wanaoamini katika wewe na naahidi kuwa Dulla mpya ambaye hatopelekeshwa tena na miluzi mingi.
“Naomba unisamehe bro na Wasafi nzima kwa ujumla naomba mnisamehe sana pia nyinyi ni famila yangu,” amesema Makabila.