×

Uso kwa uso na mtoa roho!-2

ILIPOISHIA:
“Wale ni wachawi wanaosumbua watu kijijini kwetu, naona wametangaza vita na mimi, hawanijui hawa,” alisema baba na kama ilivyotokea mara ya kwanza, aliyeyuka na kupotea eneo lile, wale wachawi nao wakapotea kwenye upeo wa macho yangu, nikasikia kelele za watu waliokuwa wakilia kwa sauti kubwa kama wanaolalamikia maumivu makali.SASA ENDELEA…

“Ndiyo dawa yao, siku nyingine wakirudia watanikoma,” alisema baba, nikashtuka tena baada ya kumuona amesimama palepale alipokuwa mara ya kwanza, pembeni yangu lakini safari hii alikuwa akihema kwa nguvu kama mtu aliyetoka kukimbia. Nilijihisi kama nipo ndotoni.

“Baba mbona sielewi kinachotoke…” nilisema lakini kabla sijamalizia kauli yangu, macho yangu yalitua kwenye mkono wa baba uliokuwa na jeraha na alama kama ameng’atwa na mnyama mkali, huku damu nyeusi zikimtoka kwa wingi.

“Ninii!” baba alinihoji baada ya kuona macho yangu yameganda kwenye mkono wake.
“Umeumia baba, pole,” nilisema lakini baba hakunijibu kitu zaidi ya kuusogeza ule mkono wenye jeraha karibu na uso wake, akawa analichunguza vizuri lile jeraha.

Akasogea pale kwenye mti wa mtangetange na kuchuma majani yake, akayatia mdomoni na kuanza kuyatafuna kisha muda mfupi baadaye, aliyatoa mdomoni na kuyabandika juu ya kidonda chake, nikamuona akifumba macho kama ishara ya kuonesha jinsi alivyokuwa akihisi maumivu.

“Nitakuwa sawa usijali, nimeshazoea kusumbuana na hawa wachawi. Inabidi na wewe uwe jasiri,” alisema baba huku akiendelea kujisafisha pale kwenye jeraha lake. Zile damu nyeusi zilizokuwa zinamtoka zikakata, akashusha pumzi ndefu na kuendelea na kazi ya kuchimba dawa.

Kwa kweli matukio yale niliyoyashuhudia yaliufanya moyo wangu uingiwe na hofu kubwa mno. Sikuwahi kudhani baba anaweza kuwa na nguvu za giza kiasi kile, siku zote niliamini alichokuwa anakifanya ni kutibu watu kwa mitishamba tu, basi! Hata hivyo, nilijikaza kiume na kuuficha mshtuko nilioupata, nikaendelea kumsaidia baba na hatimaye tukamaliza kazi yetu.

Wakati tunarudi kutoka msituni, baba alinisisitiza njiani kwamba sitakiwi kumwambia mtu yeyote kuhusu nilichoshuhudia, hata ndugu zangu wa tumbo moja. Akaniambia kwa kilichotokea, anahisi kuna madhara makubwa yatakuwa yametokea kijijini kwetu.
“Unamaanisha nini baba?”

“Wale wachawi waliotuvamia kule msituni, mmoja nimemuumiza sana sijui kama anaweza kuwa yupo hai mpaka muda huu.”
“Kwani ni akina nani wale?”

“Kwani wewe huwajui wale? Au hujawatazama vizuri?” baba alinihoji na kuanza kunifafanulia, akaniambia yule mmoja ni mzee wa kanisa pale kijijini kwetu, aliponitajia jina lake ndiyo nikamtambua vizuri. Alikuwa ni mzee Mwankuga, ambaye mara kwa mara alikuwa akiingia kwenye migogoro na baba kutokana na kugombea mpaka wa shamba kwa sababu shamba letu na lake yalikuwa yamepakana.

Nakumbuka kuna kipindi waliwahi kupelekana mpaka kwa balozi kutokana na ugomvi wao huo. Hata familia zetu hazikuwa na uhusiano mzuri, sisi tulikatazwa kabisa kuongea wala kucheza na watoto wa mzee Mwankuga na yeye hali kadhalika.
”Kwa hiyo unataka kusema mzee Mwankuga naye ni mchawi? Si mtumishi wa Mungu yule na kila Jumapili anaenda kanisani tena anakaa siti za mbele?”

“Mwanangu dunia ina mengi hii! Hutakiwi kumuamini mtu, pale kanisani waumini karibu wote huwa wanakuja kutafuta dawa kwangu, wengine wanataka wapandishwe vyeo, wengine wanataka kujikinga na wengine wana shida mbalimbali, usiwaamini binadamu,” alisema baba, nikabaki nimeduwaa. Hizo zikawa ni habari nyingine za kushangaza sana kwangu.

“Sasa pale si walikuwa wawili? Huyo mwingine ni nani?”
“Si yule mwalimu wenu, Mwashambwa?”
“Mwalimu wetu Mwashambwa anayetufundisha hesabu naye ni mchawi?” niliuliza kwa mshangao mkubwa huku mdomo nikiwa nimeuacha wazi.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano ijayo kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave a Comment