×

Kocha Yanga Awakabidhi Rungu Aziz Ki, Morrison Kuiua Simba Leo

                                                        Staa wa Yanga Aziz Ki

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amefichua kuwa amepanga kuwatumia vizuri nyota wake wapya ndani ya timu hiyo akiwemo Benard Morrison na Aziz Ki katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

 

Nabi ametoa kauli hiyo kuelekea katika mchezo huo ambao unatarajiwa kupigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar huku akiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Simba msimu uliopita katika mchezo wa Ngao ya Jamii.

 

Morrison na Azizi Ki, ni miongoni mwa mastaa wapya waliosajiliwa ndani ya kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara akiwemo kiungo wa zamani wa Newcastle United, Mrundi, Gael Bigirimana.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Nabi alisema kuwa malengo yao makubwa ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kuendeleza rekodi ya msimu uliopita kwa kuweza kushinda ngao hiyo huku akisisitiza kutoa nafasi kwa nyota wake wote wakiwemo wachezaji hao.

 

“Tunachokiangalia ni jambo la kuweza kushinda kwa kuwa hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu wao wanatujua na sisi tunawajua wao maana kila mmoja ameona alichofanya mwenzake kwenye mechi za mwisho za kirafiki lakini upande wetu, tumeangalia suala la kupata ushindi kutokana na ukubwa wa kikosi chetu.

 

“Hatuwezi kuwa na wachezaji halafu wakashindwa kutumika, sasa kila mchezaji ambaye unaona tunaye atatumika kulingana na ubora wake kuelekea kwenye mchezo huo lakini jambo kubwa ambalo tunaliangalia ni kupata matokeo ya ushindi ili kupata picha halisi ya msimu mpya ndani ya timu yetu,”

Leave a Comment