
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema kuwa moto uliozuka na kuunguza Club ya Dallas iliyo ndani ya Mwanza Hoteli umedhibitiwa huku akisema hadi sasa chanzo cha moto huo hakijulikani.
Moto huo ulianza siku ya jana Jumatano usiku saa 1:14 kisha kusambaa katika eneo lingine la jengo ilipo klabu hiyo lakini maafisa wa zimamoto mkoa wa Mwanza waliijitahidi kuuzima moto huo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo, Malima ametoa salamu za pole kwa mmiliki wa hoteli hiyo na wamiliki wa Club ya Dallas huku akiwasitiza wakazi wa mkoa huo kujenga miundombinu ya kukabiliana na majanga ikiwemo moto kwenye maeneo yao.
“Tukio hili lilitokea nikiwa katika eneo hili natoka ofisini nikawa naona moshi, kama unavyojua moshi hauchelewi kuwa moto. Hapa tuna ofisi nyingi za umma ikiwemo benki ya NMB na jengo la Benki Kuu, lakini moto huu umedhibitiwa,” amesema mkuu wa mkoa huo.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mwanza, Kamila Labani amesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha moto huo huku akisisitiza kwamba hakuna madhara kwa binadamu na wanaendelea na utambuzi wa mali zilizoteketea kutokana na moto huo.
Imeandikwa na: Oswald Mwesiga kwa msaada wa kimitandao.