
MAHAKAMA ya Wilaya Kinondoni jijini Dar es salaam, imemhukumu Dunia Suleman (36) kwa jina maarufu P squre, kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka nane.
Suleman, ambaye ni Beach Boy na mkazi wa Msasani wilaya ya Kinondoni, anadaiwa kumbaka binti huyo wakati akimfundisha kuogelea katika ufukwe wa Coco beach, uliopo Bahari ya Hindi jijini Dar es salaam, mshtakiwa huyo amehukumiwa kifungo hicho na Hakimu Mkazi Mkuu Erick Rwehumbiza baada ya kukiri shtaka lake.

Pia mahakama hiyo imetoa amri tube ya tairi ya gari iliyotumika kutendea kosa hilo iharibiwe, akitoa hukumu hiyo Hakimu Rwehumbiza alisema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.
“Mahakama imekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa baada ya kukiri shtaka la kubaka mtoto, hivyo utatumikia kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa wenzako,” alisema Rwehumbiza.
Awali Wakili wa Serikali Michael Shindai, aliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa kwa kuwa vitendo vya ubakaji watoto vimekuwa vikiongezeka kila siku.
“Mheshiwa hakimu, kwa kuwa mshtakiwa amekiri shtaka lake mwenyewe bila kulazimishwa na mtu, naomba mahakama yako itoe adhabu kali kukomesha vitendo hivi,” alidai Shindai.
Pia upande wa mashtaka uliwasilisha vielelezo vinne ambavyo ni fomu ya PF3, maelezo ya onyo ya shahidi, hati ya gwaride la utambuzi na hati ya kuchukulia mali ambayo ni tube ya tairi la gari lililotumika kutendea kosa.
Kabla ya kupewa adhabu hiyo Mahakama hiyo ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali, hata hivyo, mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na kwamba alipitiwa na shetani.

“Naomba mama wa mtoto huyu, anisamehe sana, nilipitiwa na shetani naomba msamaha,” alidai mshtakiwa.
Hakimu Rwehumbiza alitupilia mbali maombi ya mshtakiwa huyo na kumhukumu kifungo cha maisha jela, kwa mujibu wa hati ya mashtaka P square anakabiliwa na kesi ya jinai namba 183/2022.
Imeandikwa na: Oswald Mwesiga kwa msaada wa mitandao.