×

Mhandisi wa Marekani Aachiwa na Kundi la Taliban Walimshikilia Mateka Tangu 2020

Mhandisi wa Marekani, Mark Frerichs.

Kundi la Taliban limemwachilia mhandisi wa Marekani ambaye walikuwa wamemshikilia mateka tangu 2020 ili kubadilishana na kiongozi wa kikabila wa Afghanistan aliyekuwa kizuizini na Marekani tangu 2005.

 

Mark Frerichs alikabidhiwa katika uwanja wa ndege wa Kabul siku ya Jumatatu, Taliban walisema.

Kwa upande wao walimpokea Bashir Noorzai, mshirika wa Taliban anayetumikia kifungo cha maisha jela kwa ulanguzi wa dawa za kulevya.

 

Rais wa Marekani Joe Biden alisema kuwa kubadilishana kunahitaji “maamuzi magumu” ambayo hakuyachukulia kirahisi.

Bashir Noorzai aliwaambia waandishi wa habari mjini Kabul kuachiliwa kwake kutaleta amani na Marekani

Frerichs, mwenye umri wa miaka 60, alitekwa nyara na kundi la Taliban mwaka mmoja kabla ya kundi hilo kurejea madarakani nchini Afghanistan na serikali yake inayoungwa mkono na nchi za Magharibi kuporomoka.

 

Alikuwa akiishi na kufanya kazi huko Kabul kama mhandisi wa ujenzi kwa miaka 10.

Dadake Bw Frerich, Charlene Cakora, alisema familia haijawahi kukata tamaa ya kumpata tena.

“Nimefurahi sana kusikia kwamba kaka yangu yuko salama na anaelekea nyumbani kwetu. Familia yetu imesali kwa hili kila siku ya zaidi ya miezi 31 ambayo amekuwa mateka,” alisema katika taarifa.

 

“Kulikuwa na baadhi ya watu waliokuwa wakibishana dhidi ya mpango huo uliomrudisha Mark nyumbani, lakini Rais Biden alifanya kilichokuwa sawa. Aliokoa maisha ya mkongwe wa Marekani asiye na hatia.”

“Kwa hakika tunajisikia faraja sana. Imekuwa muda mrefu,” alisema.

 

Kuzuiliwa kwa afisa huyo wa zamani wa jeshi la wanamaji kumekuwa kikwazo kikubwa katika kuboresha uhusiano kati ya Marekani na Taliban, ambayo serikali yao bado haijatambulika na nchi yoyote duniani.

 

Rais Biden alisema mwezi Januari: “Taliban lazima imwachilie mara moja Mark kabla ya kutarajia kuzingatiwa kwa matarajio yake ya uhalali. Hili haliwezi kujadiliwa.”

Hata hivyo, Mmarekani mwingine mmoja amesalia mikononi mwa Taliban.

 

Kwa upande mwingine, Bashir Noorzai alikaribishwa kishujaa aliporejea katika mji mkuu wa Afghanistan, na alilakiwa na wapiganaji wa Taliban waliobeba taji za maua.

 

“Kuachiliwa kwangu pamoja na Mmarekani kutafanya amani kati ya nchi hizi,” aliuambia mkutano wa wanahabari.

Noorzai alikuwa mshirika wa karibu na rafiki wa mwanzilishi wa Taliban Mullah Omar na alisaidia kufadhili serikali ya kwanza ya Taliban katika miaka ya 1990.

Leave a Comment