
MABONDIA Twaha Kiduku na Karim Mandonga leo Septemba 21, 2022 wamepokewa kwa shangwe kubwa la wakazi wa Mtwara tayari kwa pambano la Ubabe Ubabe 2 huku wakikaribishwa na mkuu wa mkoa Kanali Ahmed Abasi Ahmed kwa kuwatakia ushindi mkubwa katika pambano la Jumamosi.

Kiduku na Mandoga ambao mkoani hapa kwa usafari wa ndege walipokelewa na mkuu wa wilaya ya Mtwara, Dustan Kyobya akiwa na madiwani pamoja na wananchi walijitokeza katika mapokezi hayo kabla ya kufika kwa mkuu wa mkoa ambaye alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha mabondia hao.

Pambano hilo ambalo limepangwa kufanyika katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona uliopo mkoani Mtwara chini ya udhamini wa Gazeti la Spoti Xtra, +255 Global Radio, Smart Gin, Creative Bee, Azam TV, Robby one pharmacy, H Fm, Swahili Water, Shujaa FM na Bongo Boxing Safari App huku kiingilio kikiwa ni Sh 5000 kawaida, Sh 10,000 VIP B na Sh 20,000 kwa VIP A.

Mabondia hao ambao walipitishwa katika mitaa mbalimbali ukiwemo katika mji mkongwe wa mikindani, soko kuu, chuo na stendi kuu ya mabasi Mkanaledi kabla ya kwenda kwa mkuu wa mkoa, Kanali Ahmed Abasi Ahmed ambaye aliwakaribisha mkoani hapa na kuwatakiwa ushindi kwenye pambano hilo la kimataifa huku akiwataka kutembelea vivutio vya kitalii vinavyopatikana mkoani hapa.
Kwa upande wa Kiduku na Mandonga wameshukuru mapokezi hayo pamoja na kamati yote ya maandalizi ambapo kila mmoja ameahidi kutoa zaidi ya ushindi siku ya Jumamosi.
Stori: Ibrahim Mussa