
MASTAA wa Yanga leo watakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha kuwa wanapata matokeo mazuri katika mchezo wao wa kwanza wa makundi wa Kombe la Shirikisho wakiwa huko nchini Tunisia.
Yanga watashuka katika Uwanja wa Olympic Rades wa nchini Tunisia ambao ni uwanja wenye kumbukumbu kwa Yanga kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Club Africain walishinda kwa bao 1-0 na kutinga makundi.
Kueleka katika mchezo huo tayari Spoti Xtra limefanikiwa kupiga stori na baadhi ya wachezaji kabla ya mchezo huo ambapo waliweza kuuzungumzia mchezo huo kama ifuatavyo.

FISTON MAYELE
“Ni mchezo wetu wa kwanza wa ugenini, malengo yetu ni kupata matokeo mazuri tukiwa ugenini, tunafahamu tuna jukumu kubwa kutokana na ubora wa wapinzani wetu hivyo haitakuwa kazi nyepesi kwetu.
“Tayari kama wachezaji tupo tayari kwa mchezo huu lakini tupo tayari kuhakikisha tunaipambania timu ili iweze kufika mbali, uzuri kwa sasa wote sio wageni tena kwenye haya mashindano.”
DICKSON JOB
“Tunayo historia nzuri huku Tunisia lakini hilo kwa sasa sio muhimu tena, muhimu ni kuweza kupambana tena na kuweza kuipa matokeo mazuri timu,mashabiki wanatakiwa kutuunga mkono katika kila hatua ambayo tumefikia.
“Yanga tunahitaji kufanya vyema na kufika mbali katika michuano hii, malengo yetu ni kufika robo fainali, lazima tujiandae na tuanze vyema ili tufanikishe malengo.”

KIBWANA SHOMARI
“Safari yetu ndio inaanza tunaamini tulianza vyema na tutaimaliza vyema, kama unavyofahamu lengo la kwanza kwa upande wetu lilikuwa ni kufika makundi ,tunashukuru tumefika hapo.
“Kwa sasa tunatazama lengo la pili ambalo ni kufika robo fainali,sasa kama tutashindwa kupambana katika viwanja hivi vigeni basi tutakuwa katika wakati mgumu,lazima tufanikishe kuanzia mwanzo mpaka mwisho, tunaimani tutaanza vizuri.”
FARID MUSA
“Wapinzani wetu ni wazuri, wanacheza mpira wa kasi na wamekuwa na takwimu nzuri za kufunga mabao, kwa upande wetu tumejiandaa kucheza na wapinzani wetu sisi kama wachezaji.
“Yanga mara zote tumekuwa na mashabiki bora ambao wamekuwa bega kwa bega na sisi wachezaji kuhakikisha kuwa tunafikia malengo yetu kwa pamoja, tunawaahidi tukiwa huku Tunisia kuwa tunapambana na tunaanza na mchezo wetu vyema kwa kupata matokeo mazuri.

DJUMA SHABANI
“Tunafahamu tunakwenda kucheza na timu ya aina gani,bahati nzuri kwa sasa tayari tunauzoefu mkubwa na michezo hii ya ugenini,hapo mwanzo kuna changamoto kidogo zilitukumba kucheza ugenini lakini kwa sasa jambo hilo halipo tena.
“Hivyo kilichobaki kwa sasa ni kucheza, wachezaji tayari tumepewa mbinu zetu na benchi la ufundi kuona ni namna gani tutaweza kucheza na kupata matokeo mazuri, tunaomba mashabiki waendelee kutuombea.
ZAWADI MAUYA
“Tupo Tunisia kwa kazi moja tu nayo ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika huu mchezo, wachezaji tunautaka huu mchezo kwa kiasi kikubwa, tumejiandaa vizuri na tunaamini pia tutakwenda kufanya vizuri,muhimu ni sisi tuweze kupata matokeo ya ushindi.
LOMALISA MUTAMBALA
“Tunaamini kupitia huu mchezo utatoa mwanga mzima wa safari yetu ya makundi, hivyo na sisi tunamalengo ya kuhakikisha kuwa tunaanza vyema ili tuwe na mwanga mazuri katika michuano hii, bado tunatamani kuona tunafanya makubwa zaidi.
JESUS MOLOKO
“Wachezaji tunayo malengo yetu ukiachana na yale malengo ya timu kiujumla,tunatamani kuona tunakuwa miongoni mwa wachezaji ambao watakuwa na rekodi nzuri katika michuano ya kimataifa.
“Hivyo lazima tupambane, tunafahamu kucheza mechi za ugenini,tunafahamu tunatakiwa tufanye nini katika michezo hii ya ugenini, sisi tutaifanyia kazi kama ambavvo tumeelekezwa na benchi letu la ufundi,”alisema mchezaji huyo.
0-1
Yanga alishinda ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Club Africain ya Tunisia katika hatua ya mtoani ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Stori Na Marco Mzumbe