×

Uongozi wa Yanga Watamba Kucheza robo Fainali Kombe la Shirikisho Afrika

Rais wa Yanga Eng.Hersi

UONGOZI wa Yanga, umewaambia mashabiki wa timu hiyo kwamba, wasiwe na presha yoyote kwani chama lao litacheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Yanga ipo nafasi ya pili kwenye Kundi D la michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ikiwa imekusanya pointi nne, baada ya kucheza mechi tatu, ikishinda moja, sare moja na kupoteza moja.

Akizungumza mara baada ya mchezo dhidi ya Real Bamako uliochezwa juzi Jumapili nchini Mali na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema kwa hesabu walizonazo kila kitu kinakwenda sawa.

“Mwananchi usiwe na mashaka kwa pointi moja ambayo tumepata ugenini, hii sio mbaya, ni mwanzo mzuri kwetu, tunakwenda kuweka historia mpya kwa kutinga hatua ya robo fainali.

 

“Tumedhamiria na wachezaji wapo tayari kwa ajili ya kazi kubwa na ngumu hasa kwa mechi zetu mbili Uwanja wa Mkapa, tunapambana kupata pointi sita ili kusonga mbele, hapo hesabu zitajibu.

“Ninaona wapo ambao wameanza kukata tamaa, hilo wasiwe nalo kabisa, Wananchi watembee kifua mbele, tunafanya kazi kubwa kufikia malengo yetu, lazima tushirikiane,” alisema Kamwe.

Mechi tatu zilizosalia za Kundi D, Yanga itacheza mbili nyumbani dhidi ya Real Bamako na US Monastir ambapo Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amedhamiria kuwashushia vipigo wapinzani wake hao.

Baada ya hapo, itakwenda DR Congo kumalizana na TP Mazembe katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo, huku hesabu za Yanga ni kuona inashinda mechi mbili zijazo ili kufikisha pointi kumi wanazoamini zitawavusha kwenda robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA

EXCLUSIVE: SALEH JEMBE AFICHUA MPASUKO SIMBA, SARE ya YANGA – ”MANGUNGU HAWEZI KUWA YANGA”…

Leave a Comment