
Rais William Ruto wa Kenya Jumatatu alipokea ombi la pamoja la Kenya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 pamoja na majirani Uganda na Tanzania.
Waziri wa Michezo wa nchi hiyo Ababu Namwamba na Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya Nick Mwendwa waliwasilisha hati hiyo kwa Dkt Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Kenya imeungana na majirani wake Tanzania na Uganda katika mpango uliopewa jina la “Pamoja” kuleta mashindano ya bara hilo yanayotamaniwa sana katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza katika historia.
Rais alimuagiza Waziri wa Michezo Ababu Namwamba kuwasiliana na wenzake kutoka Uganda na Tanzania ili mataifa hayo matatu ya Afrika Mashariki yaweze kufanikiwa kushinda ombi la kuandaa mashindano hayo makubwa zaidi ya kandanda barani.