
UONGOZI wa Simba SC, umesema kwa sasa akili zao wanazielekeza kwenye michuano ya CAF Super League na tayari wameshaanza maandalizi ya michuano hiyo, ambayo kwa mara ya kwanza itaunguruma mwaka huu 2023.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kuwa, wakati viongozi, watu wa skauti na makocha wakiangalia wachezaji wa kuwasajili, mazoezi yanayofanyika sasa ni maandalizi ya Super League pamoja na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2023/2024.

“Tayari tumeshaanza maandalizi ya msimu ujao, haya yanayoendelea ni maandalizi kwa ajili ya mashindano yajayo pamoja na ligi kwa sababu msimu mpya unaanza hivi karibuni.
“Kama tulivyosikia msimu ujao utaanza kwa mechi ya Ngao ya Jamii itakayochezwa kwa mfumo wa timu nne, kwa hiyo lazima tuanze maandalizi na michuano ya CAF msimu ujao itaanza mapema sana, tuko makini ndiyo maana tumeamua kuanza mipango mapema,” alisema Ahmed.
Alisema pamoja na kwamba wachezaji wao wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi mbili za mwisho wa Ligi Kuu Bara, lakini makocha wanatumia muda huohuo kuandaa kikosi cha msimu ujao na kuangalia wachezaji wa kuendelea kufanya nao kazi.
STORI: HAPPNESS LAURENT