ILIPOISHIA GAZETI LA RISASI JUMATANO:
Mara nikasikia ikiingia bafuni, nikasikia kukohoa. Mkohowo huo ulitaka kufanana na wa afande Mwira. Nikatulia kimya na kufuatilia ili nijue ni nani!
“Ee nivumiliee…nakupenda sana wewe…hata moyo wangu eee…” aliimba na ndipo nikajua ni nani sasa…
“Mh!” niliguna. Moyo ukaanza kwenda mbio. Nilijua nimeumbuka…
CHECHEMEA NAYO…
Ilipita kama sekunde kadhaa, nikasikia maji yakimwagika, mtu akiwa anaoga.
Nikajua mtu huyo hawezi kutoka muda huo, nikatoka mbio hadi chumbani kwa yule afande mbaba, nikamkuta amesimama eti alitaka kunifuatilia chooni maana nilichukua muda mrefu.
Kulipokucha, baadhi ya maafande walishaondoka kwenda kazini, lakini afande Mwita alibaki. Afande yule mbaba pia alibaki.
Saa moja juu ya alama, afande Mwita akaja kumgongea afande wangu mbaba…
“Mura,” aliita afande Mwita. Sijui mura maana yake nini!!
Jamaa naye huku chumbani akaitika kwa kusema neno hilohilo.
“Upo?” aliuliza afande Mwita…
“Nipo mura…vipi, hujuenda kazini leo?”
“Bwana nina msala…”
“Msala gani tena?”
Afande Mwita akamsimulia mwenzake kuhusu kisanga chake chote…
“Mura…hivi ninavyokwambia sasa hivi hapa nawaza. Je, mama yake akija sasa hivi itakuaje? Nitamwambia binti yake yuko wapi?”
“Daa! Mura hapo kweli umeshikwa pabaya. Ni kuomba Mungu, maana isijekuwa alipotoroka amekumbana na majambazi ameuawa, itakula kwako mura.”
Walipitisha ukimya kila mmoja akitafakari, mimi nikashikwa na hali ya kutaka kupiga chafya! Ilibidi nijizuie kwa nguvu zangu zote mpaka nikachukua shuka na kulitumbukiza kinywani ili tu nisipige chafya. Nikafanikiwa.
Baadaye afande Mwita alirudi chumbani kwake, afande wangu mbaba naye alirudi kitandani akiwa anafunga mlango…
“Da! Jamaaa anasumbuka sana. Angejua upo ndani kwangu sijui ingekuwaje? Angenifyatua na risasi,” alisema afande wangu.
Mimi niliachia tabasamu tu kwani dhamira ilinisumbua kuona mtu hakulala kisa mimi na kumbe nipo sehemu ya usalama kabisa…
“Sasa mimi nitatokaje?” nilimuuliza afande wangu kutaka kujua…
“Ala! Sasa uondoke kwenda wapi mpenzi wangu? Hapa umefika! Mimi nikienda kazini nakufungia ndani mpaka nitakaporudi. Yaani wewe na mimi ndiyo tumeshakuwa mke na mume tayari.”
Niliogopa kusikia hivyo kwani nilijua mazingira yatakuwa magumu sana. yaani nikae chumbani mchana kutwa au usiku mwingine nikimsubiri yeye, ngumu sana!
***
Nyumba ilikuwa kimya sana, afande Mwita aliondoka na afande wangu pia aliondoka. Yeye afande wangu aliondoka baada ya kupika ubwabwa na nyama akaniachia, eti nikijisikia njaa nile.
Nilikuwa nimepitiwa na usingizi wa asubuhi baada ya ule wa usiku kuamkia asubuhi. Nadhani mnaujua. Yaani watu wakiamka asubuhi, baadaye kama watakuwa bado kitandani lazima wapitiwe na kausingizi kengine ka mwishomwisho!
Nilishtuliwa na mlango mkubwa kugongwa…
“Ngo ngo ngo…hodi!” Ilikuwa sauti ya kiume, nikajua siyo mama. Awali nilijua ni mama amenijihimia.
Sikuamka, niliendelea kumsikiliza lakini ikafika mahali hodi hiyo ikawa ni kero sasa. nikatoka kitandani, nikafungua mlango na kwenda hadi mlango mkubwa lakini nilikwenda kwa kunyata ili kuchunguza kwanza…
“Ngo ngo wenyewe hodi humu ndani,” ile sauti iliendelea kuita baada ya kugonga.
Nilipata upenyo na kuangalia nje kupitia nafasi ya mlango, kipande cha mbao na kipande kingine. Niliwaona wanaume wawili wamesimama.
Nilisonya, nikarudi zangu ndani, chumbani, nikapanda kitandani kulala. Sikumbuki waliondoka muda gani, lakini nilishtuka mimi saa sita na nusu baada ya simu yangu kuita sana. Nilitoka kitandani na kuifuata ilipo. Alikuwa afande wangu, mbaba maana si nilimsevu siku ya kwanza kabisa…
“Haloo…”
“Dear hujambo?” alinisalimia…
“Sijambo, mzima wewe?”
“Mimi mzima, umeshaamka wewe?”
“Khaa! Sasa ningekuwa sijaamka, ningepokea simu? Si ningekuwa bado usingizini,” nilimuuliza…
“Kumbe wewe jeuri ee? Basi kuna siku utakula jeuri yako, mimi nipo kazini, take care hapo nyumbani, nimegundua umebaki peke yako,” aliniambia kwa sauti yenye amri…
Wakati tunaongea, nikasikia mlango wa uani ukifunguliwa, nikakata simu haraka sana bila kumwambia kwa nini nakata simu.
Nikatoka kitandani, nikatembea hadi mlango wa chumbani, nikatulia hapo kimya kabisa! Aliyefungua mlango nikasikia anaufunga, kwarakachakwarakacha.
Nikaogopa, sikujua ni jambazi au mtu wa aina gani! Mara nikasikia mlio wa viatu kutembea…ko…ko…ko! Nilitetemeka.
Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Risasi Jumatano.