×

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa – 40

ILIPOISHIA:

Destiny akiwa Tanzania kulifuatilia Kundi la Wab, kupitia vyombo vya habari anasikia kuwa kundi hilo lingefanya uhalifu wa kutisha kwenye moja ya sehemu muhimu jijini Dar es Salaam siku iliyofuata.

Kwa akili za kujiongeza, Destiny anajenga mazingira ya kufanyika kwa tukio hilo hospitalini jambo ambalo rafiki yake Elizabeth halikumuingia akilini pale alipomwambia.TAMBAA NAYO…

MASHAKA ya Elizabeth hayakumzuia Destiny kupanga mipango juu ya alichokuwa anawaza, akili yake ilikuwa imeshafanya kazi zaidi ya uwezo wa kawaida.

Kutokana na kufuatilia msururu wa matukio ya Kundi la Wab, msichana huyo alifahamu kwa vyoyote vile akina Mtima wangefanya shambulio kwenye hospitali yoyote kubwa ili kuacha maumivu makali kwa jamii.

Asubuhi ya siku iliyofuata walikuwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wamekaa sehemu ambayo hakuna aliyefahamu kama kulikuwepo na waandishi wa habari, huko ndiko Destiny alikomwambia Elizabeth kuwa alifikiri kwa asilimia 70 tukio hilo lingefanyika.

Wakiwa wamekaa eneo hilo, saa zilizidi kukatika lakini hadi saa moja jioni Kundi la Wab halikuweza kufika na wala hawakuwa wamesikia mahali popote kumetokea uhalifu.
“Sidhani kama kuna jambo lolote litatokea Destiny?” Elizabeth alisema.
“Kwa nini?”

“Muda unazidi kwenda na hakuna dalili!”
“Kuwa mvumilivu, dakika moja ni kubwa sana katika nyakati.”
Hakukuwa na namna, Elizabeth akawa mpole, wakazidi kusubiri lakini hadi saa tano za usiku, hakuna lolote lililokuwa limetokea, wote wakakata tamaa juu ya uwezekano wa kutokea kwa tukio hilo.

Wakati huo, eneo zima la Hospitali ya Muhimbili lilitawaliwa na ukimya wa hali ya juu ambapo kwenye wodi za wagonjwa manesi wa zamu walikuwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Hakuna aliyekuwa na wasiwasi juu ya jambo lolote lile kutokea, lakini ghafla ilipotimu saa 5: 59 mlipuko mkubwa ukatokea eneo hilo, ulikuwa ni wa mabomu, majengo yakaanza kushika moto na kudondoka, jambo lililosababisha kelele kuanza kusikika kutoka kila kona ya eneo hilo.

Destiny na Elizabeth wakiwa sehemu wamejibanza wanaushuhudia mlipuko huo, bila kutegemea jengo kubwa lililokuwa pembeni yao lilianza kuporomoka, walijaribu kuinuka ili wakimbie kujiokoa bila mafanikio, jengo hilo liliwafunika.

Ghafla hali ya taharuki ilitawala eneo zima la Hospitali ya Taifa Muhimbili, vingo’ra vya polisi vikaanza kusikika vikielekea katika eneo hilo, magari ya zima moto na watu wengi kutoka mitaa ya karibu ikiwemo Upanga, Jangwani, Magomeni na Kariakoo walianza kumiminika katika hospitali hiyo.

Kila mmoja alikuwa anashangaa na kujiuliza nini kilitokea hadi ukazuka moto uliosemekana kusababishwa na mlipuko wa mabomu, lakini hakuna aliyepata jibu, lilikuwa ni fumbo la kila mmoja.

Vikosi maalum vya zima moto viliendelea kufanya kazi yake ya kuhakikisha moto unazimika, pia kikosi kilichovalia mavazi maalum yasiyoruhusu moto kupenya wala hewa ya Atomic Monoxide iliyosababishwa na mlipuko huo wa mabomu vilizidi kuichomoa miili ya watu waliokuwa wameangukiwa na majengo ya hospitali hiyo huku wengi wao wakionekana kuungua vibaya mno.

“Huu ni ugaidi mkubwa kuwahi kutokea nchini!” Inspekta Thomas Rwempashana aliongea huku akitikisa kichwa.

“Lakini afande jana kundi la kigaidi la Wab lilitangaza kufanya uhalifu.” Meshaki Zombi, moja ya madaktari waliokuwa wanafanya kazi hospitalini hapo aliyefika muda mfupi baada ya kutokea kwa tukio hilo alimwambia.

“Ni kweli, lakini ilikuwa ni vigumu kufahamu wapi tuweke ulinzi na wapi tuache.”
“Kwa nini msingeweka katika maeneo yote muhimu.”
“Ni kosa tumefanya.”

“Uzembe kama huo unagharimu sana kiongozi, ona kilichotokea!” Baada ya maneno hayo ya Dk. Zombi, Inspekta Rwempashana alikosa neno la kuongeza.
Ukweli ni kwamba hali ilikuwa inatisha, mpaka wakati huo miili ya marehemu waliounguzwa vibaya kwa moto takriban 200 ilikuwa imepangwa katika uwanja wa wazi wa hospitali hiyo huku ikiwa ndani ya mifuko ya naironi.

Kwa upande wa wananchi walizidi kugubikwa na hali ya sintofahamu, hali kama hiyo iliyotokea walizoea kuiona kwenye nchi zenye machafuko kama Somalia na Sudan, kutokea Tanzania ilikuwa ni alamu tosha iliyowafanya wakumbuke umuhimu wa kuchukua tahadhari.

Je, nini kitaendelea? Destiny na Elizabeth wamekufa? Ni Wab waliofanya ugaidi huo? Usikose wiki ijayo.

Leave a Comment