×

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-36

ILIPOISHIA WIKIENDA
Alikuwa amemlaza mtoto kitandani kwake, nikaenda kuugusa mwili wake.
“Kweli mwili uko moto,” nikasema.
Mke wangu naye akaja kumshika kwenye kichwa.
“Jibichwa limotoo.”

“Mpeleke hospitali.”
“Nilikuwa nakusubiri wewe urudi nimpeleke.”
Tukamuita dereva, mke wangu na mtoto pamoja na mtumishi wetu wakapakiwa kwenda hospitali.
SASA ENDELEA…

Baada ya saa mbili walirudi.
“Daktari amempima malaria lakini amesema hana malaria,” mke wangu akaniambia.
“Sasa atakuwa ana nini, kitu gani kinampandisha joto?”
“Amenipa dawa hizi nimpe, ameniambia akinywa joto litapungua.”
Alinionesha pakiti iliyokuwa na tembe za kumeza za watoto.
“Ale tembe ngapi?”

“Tembe moja tuivunje mara mbili. Ale nusu moja kutwa mara mbili.”
Mke wangu akamtayarishia kipande cha tembe moja ambacho alikisaga na maji kwenye kijiko kisha akamnywesha.
Lile joto baadaye lilipungua. Lilibaki kidogo tu kwenye kichwa. Tukapata matumaini kuwa hali hiyo itaondoka.

Kabla ya kwenda kulala usiku nilisali sana. Mke wangu alikuwa akinitazama. Mwanamke huyo hakuwahi kuniona hata siku moja nikisali chumbani mwangu. Kanisani kwenyewe nilikuwa nikienda siku mojamoja. Aliyekuwa akienda kanisani siku za Jumapili aghalabu alikuwa ni yeye.

Uchawi na ibada wapi kwa wapi!
Bila shaka usiku ule mke wangu alinishangaa kuona ninasali. Hakujua ni kwa nini siku ile nilikumbuka kusali. Kusema kweli nilisali kwa sababu ya tatizo la mwanangu. Sikutaka wale wachawi wafike tena nyumbani kwangu.
Baada ya sala hiyo iliyochukua karibu nusu saa tukalala.

Usingizi ulikuwa mtamu kutokana na matumaini niliyoyapata kwa ile sala. Lakini nilikuja kuamshwa usingizini kwa kelele kama zile zilizotokea usiku wa jana yake.
Nikatazama saa yangu na kuona ilikuwa saa nane na nusu usiku.

Nyumba yangu ilikuwa imezungukwa na wachawi waliokuwa wakipiga kelele wakisema wanamtaka mtoto wao.
Moyo wangu ulishituka sana na kupata hasira. Kumbe sala yangu haikusaidia chochote. Ni kwa vile nilikuwa mwenzao au ni kutokana na kosa langu la kumkumbuka Mungu wakati wa shida tu?

“Hawa watu laana kweli!” nikalaani kwa sauti ya kusikika na kuinua uso wangu kutizama kwenye dirisha.

Dirisha lilikuwa la vioo na liliwekewa mapazia ambayo yalikuwa yamekunjuliwa na kuliziba dirisha hilo. Hata hivyo, niliweza kuona vivuli vya watu waliokuwa wakipitapita.
“Hawa nikiwasemesha ndiyo nitakuwa nimewachokoza, bora ni kuwanyamazia tu,” nikajisemea huku nikiomba Mungu mke wangu asiamke.

Baadaye kidogo niligundua kuwa wachawi hao hawakuwa wakiizunguka nyumba yangu tu, bali walikuwa wakifanya vitendo vyao vya kichawi. Walifanya katika pembe zote za nyumba yangu. Nilikuwa na hakika kwamba asubuhi ningekuta makimba waliyoyaacha.
Walikuwa wakinifanyia uchawi huo kwa ajili gani?
Kwa ajili ya kumchukua mwanangu? Nikajiuliza.

Wakati najiuliza hivyo Mkanga alishituka usingizini ghafla akaanza kulia kwa kelele.
Mama yake akaamka hapohapo. Wakati anamtazama mwanawe akazisikia zile sauti za wachawi.

“Baba Mkanga kuna nini huko nje?” akaniuliza kwa wasiwasi.
Sauti yake ilisikiwa. Kabla ya kumjibu, ikajibiwa huko uani.
“Tunamtaka mtoto wetu!”
“Baba Mkanga ni kina nani hao?”
“Sijui,” nikamjibu.

“Kwani wewe huzisikii hizo sauti?”
“Nazisikia.”
“Hujui ni kina nani?”

“Tunamtaka mtoto wetu!” Ile sauti ikasikika tena kutoka nje ya dirisha.
“Nyinyi ni kina nani?” Mke wangu akawauliza kwa ujasiri.
“Muulize mume wako, sisi ni wenzake,” sauti ikamjibu.
“Nyinyi ni wenzake mume wangu?”
“Ndiyo.”

“Mnatoka wapi?”
“Tunatoka Kijiji cha Mbogwe huko Nzega.”
“Sasa mmefikaje hapa usiku huu?”
“Tunamtaka mtoto wetu.”

“Mtoto wenu yupi?”
“Anamjua mume wako, leo tutamchukua tu.”
Mke wangu alitaharuki akainuka na kuketi kitandani.
“Hao ni kina nani,” akaniuliza kwa ukali.

“Nimekwambia kwamba siwajui.”
“Anatujua, sisi ni wenzake. Tulikuwa tukifukua makaburi pamoja. Ana deni letu la mtoto. Alituambia akizaa mtoto wa kwanza atatupa sisi tumle!”
“He! Mume wangu…vipi?”

1 Comment

Leave a Comment