CATARINA yuko ndani ya chumba na amepitiwa na usingizi lakini ghafla anasikia sauti ya mtu akisogelea chumba chake na ananyanyuka na kwenda kuchungulia ili aangalie ni nani hapo ndipo anakutana na burungutu la dola likirushwa mlangoni mwake anainama na kuziokota huku akitokeza nje ya mlango kuangalia ni nani aliyefanya hivyo.
Macho yake yanamwona Jackson Motown tajiri mtoto aliyeongea naye jana yake kwenye simu akimweleza juu ya hisia zake. Anafunga mlango na kuketi kitandani bado akiwa na maswali mengi, akiwa hapo anaona barua ndogo iliyoambatana na burungutu hilo la dola anafungua na kusoma anashangazwa na ujumbe wa mwanaume huyo tajiri.
Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…
CATARINA aliisoma barua hiyo na kubaki na mshangao kwa nini Motown alikuwa akiongea kwa kujiamini kiasi hicho kwamba siku moja angekuwa mke wake, aliiona hiyo kama dharau na kama mwanamke wa Kiafrika aliwachukia sana wanaume ambao hawakuheshimu wanawake kwa sababu tu wao walikuwa matajiri, siku zote alipenda kuheshimiwa na kuonyeshwa upendo wa kweli hata kama mwanaume alikuwa ni masikini.
“Kamwe haitawahi kutokea, kama anaringia utajiri wake basi hapa ni kikomo, hatanipata ng’o! Bikira yangu namtunzia Kevin, mwanaume pekee anayeistahili, aliyeniokoa dhidi ya kifo.” Catarina alitamka maneno hayo akiyaapia.
Akaketi kitako kitandani na kuanza kuziangalia noti za dola miamia ambazo Motown alimrushia, moyoni mwake akakiri hakuwahi kukutana na kiasi kikubwa namna hiyo kilichoitwa chake, akaahidi kuziweka benki mara tu akishafungua akaunti na nyingine angechukua na kununua zawadi kwa ajili ya wazazi wake na Kevin, tukio hilo peke yake lilionyesha ishara kuwa kazi aliyokuwa amekuja kuifanya ilikuwa na utajiri mkubwa.
Saa mbili na nusu asubuhi Craig Anderson alifika na simu ikapigwa kutoka mapokezi akitaarifiwa, akamruhusu apandishe chumbani kwake ambako alikuwa akimsubiri baada ya kumaliza kujiandaa, Craig ndiye alikuwa na ratiba nzima ya siku hiyo.
“How are you doin’ baby?” (Unaendeleaje mpenzi?)
“I am just cool!” (Niko poa tu.)
“How was your night?” (Usiku wako ulikuwaje?)
“Anybody disturbing?” (Mtu yeyote anayesumbua?)
“Nobody!” (Hakuna mtu!)
“Are you sure?” (Una uhakika?) aliuliza Craig huku akitabasamu.
“Sure, nobody, I had a sound sleep!” (Hakika, hakuna, nililala usingizi mzuri!)
Catarina hakuwa tayari kuweka wazi juu ya Motown wala fedha alizokuwa amepewa, alifanya hivyo kwa sababu alishahisi Craig alikuwa pia akisumbuliwa na hisia za mapenzi juu yake, hivyo hakutaka kumuumiza moyo. Kilichomshangaza ni jinsi alivyouliza mara mbili na kwa uhakika kama vile alikuwa na taarifa ya usumbufu alioupata usiku.
Saa nne na nusu baada ya kupata kifungua kinywa pamoja, waliondoka kuelekea ofisi za Fonex Modelling ambako Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya uanamitindo, Teddy Khumalo, aliyewahi kuwa mwanamitindo maarufu duniani raia wa Afrika Kusini ambaye baada ya kustaafu uanamitindo alirejea nyumbani kwao na kuanzisha kampuni hiyo kubwa duniani alitaka kumwona.
Mapokezi kwenye jengo kubwa la Fonex Modelling lililoko katikati ya Jiji la Johannesburg jirani kabisa na ofisi za makao makuu ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini, yalimshangaza Catarina, zulia jekundu lilikuwa limetandakwa na warembo wengi waliokuwa chini ya kampuni hiyo walikuwa wamekusanywa kumsubiri yeye, walipangwa mistari miwili kutokea kwenye gari kuingia ofisini kando ya zulia.
Catarina akapita katikati yao akirushiwa maua meupe kama ambavyo hufanyika wakati wa harusi, waandishi wa habari walikuwa makini wakipiga picha za kila tukio, machozi yalikuwa yakimtoka Catarina akiwa haamini kilichokuwa kikiendelea, moyoni alikuwa akimshukuru Mungu kwa kumpa uzuri ambao hakuununua.
“Wow! Craig where did you get this ruby from?” (Wow! Craig umeipata wapi hii Rubi?) ilikuwa ni sauti ya Teddy Khumalo akimkumbatia Catarina, hakuuficha mshangao wake, pamoja na yeye kuwa mrefu, Catarina alimzidi kwa inchi kadhaa.
“That’s a Tanzania product!” (Hiyo ni mali ya Tanzania!)
“I can’t believe Tanzania women a beautiful! Oh my God! Look at her skin, so soft! The lips, nose, neck are killing me, girl you are going to make a lot of money in this industry if only you become careful!” (Siwezi kuamini wanawake wa Kitanzania ni warembo kiasi hiki! Oh Mungu wangu! Angalia ngozi yake, laini mno, midomo, pua na shingo zinaniua, binti kama utakuwa makini, utapata fedha nyingi sana kwenye tasnia hii!)
“Thank you!” (Ahsante!) Catarina alijibu akitabasamu.
“What is your name my girl?” (Jina lako ni nani?)
“Catarina David!”
“How old are you?” (Una umri gani?)
“Sixteen this September!” (Nitakuwa na miaka kumi na sita Septemba hii!)
“You are welcome, I will do everything I can to promote you nationally and internationally!”(Karibu sana, nitafanya kila kitu ninachoweza kukutangaza kitaifa na kimataifa!)
“Thank you mom!” (Ahsante mama!)
Waliketi chini na kuanza kunywa vinywaji huku wakiongea mambo mbalimbali, huku Teddy Khumalo akimsimulia uzuri na ubaya wa tasnia ya uanamitindo hasa juu ya pombe, umalaya na matumizi ya dawa za kulevya. Catarina alimhakikishia mwanamke huyo kwamba alikuwa ni binti anayejitambua, aliyekuja nchini humo akifahamu vizuri sababu ya kuwa hapo.
“Wote huwa wanasema hivyo!”
“Nakuahidi!”
Baadaye wanamitindo wote waliitwa ndani, Catarina akatambulishwa mbele yao kwamba baada ya miezi mitatu akimaliza mafunzo kwenye Chuo cha Uanamitindo cha Johannesburg angeanza kufanya nao kazi, akiwaangalia machoni wasichana hao Catarina aligundua kabisa baadhi yao hawakufurahishwa na ujio wake ingawa hakuelewa ni kwa sababu gani, chuki ilionekana dhahiri.
Baada ya zoezi hilo alipigiwa simu mkurugenzi wa kampuni ya kupiga picha iliyoitwa South Africa Photo Catchers, bwana John Dunhill, raia wa Uingereza aliyekuwa akiishi na kufanyakazi nchini humo, yeye pia alipomwona Catarina alipagawa, hapohapo akaamua wafanye zoezi la kupigapicha kwenye chumba maalum cha kupigia picha kilichokuwa ndani ya jengo la Fonex Modelling Agency.
Catarina hakuhitaji maandalizi, hivyohivyo alivyokuwa ilitosha, John Dunhill alihitaji kupata picha akiwa kwenye mwonekano wake wa kawaida, picha nyingi zilipigwa akiwa kwenye mavazi mbalimbali, iliyowavutia zaidi ni ile aliyopiga akiwa amevalia vazi la kuogelea, iliwachanganya akili, Catarina alionekana mzuri mno, haikuwa rahisi hata kidogo kuamini alitokea Tanzania.
“This single photo will shake the fashion world, I am going to sell it to FHM Magazine!” (Hii picha moja itautikisa ulimwengu wa mitindo, nitaiuza kwenye jarida la FHM!) alisema John Dunhill akitabasamu, alikuwa kama mtu aliyekutana na bahati.
Picha hiyo moja ilinunuliwa kwa dola laki moja na Jarida la FHM, wiki mbili baadaye na mwezi uliofuata Catarina alikuwa mbele ya jarida hilo maarufu duniani kwa mitindo, ambalo wanamitindo wengi huhangaika kukaa kwenye ukurasa wake wa mbele bila mafanikio, mauzo yake yakawa makubwa mno, jina la Catarina likasambaa dunia nzima akitajwa kama mwanamitindo mpya kwenye ulimwengu huo.
Kampuni mbalimbali za mitindo duniani zilianza kuwasumbua John Dunhill, Teddy Khumalo na Craig Anderson wakimtaka Catarina kwa gharama yoyote ajiunge nao, si kampuni za mitindo tu matajiri kutoka sehemu mbalimbali duniani ambao kazi yao ilikuwa ni kuchagua warembo kwenye jarida hilo na kuwapata kwa gharama yoyote walimsumbua Craig Anderson.
“Meeeen! I saw her on the cover FHM!” (Mshkaji! Nilimwona kwenye ukurasa wa mbele wa jarida la FHM!)
“Yeah!” (Ndiyo!)
“How can I have her?” (Naweza kumpataje?)
“Mr. Motown, cool down, be a little patient, I have told you she will one day be yours!” (Bwana Motown, tulia, kuwa mvumilivu kidogo, nilishakuambia siku moja atakuwa wako!)
“Tell me any amount of money, but I want her here in New York now! I can send a private jet for her.” (Niambie kiasi chochote cha fedha, lakini namtaka awe hapa New York sasa hivi, naweza kutuma ndege binafsi!)
“I will work on it!” (Nitalifanyia kazi!)
Je, nini kitafuata katika ulimwengu wa Uanamitindo kwa Catarina? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/