ILIPOISHIA:
Shambulio la kutisha linatokea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, majengo yote yanabomolewa kwa kulipuliwa na mabomu, watu wengi waliokuwepo eneo hilo wanapoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa vibaya, miongoni mwa maiti wengi waliolala ardhini na majeruhi walikuwemo Destiny na Elizabeth.Tambaa nayo…
KIPINDI ambacho harakati za uokoaji kwa majeruhi waliotokana na shambulizi lililofanywa na Kundi la WAB zikiendelea hospitalini hapo Muhimbili, Mtima na Abdulrahman walikuwa miongoni mwa watu waliofurika hospitalini hapo kushuhudia nini kilikuwa kimetokea, wakiwa wameliegesha gari lao katikati ya magari mengi yaliyokuwa eneo hilo.
Abdulrahman alionekana kufurahia sana kilichokuwa kinaendelea huku akijipongeza kwa kujigamba juu ya kile walichokuwa wamekifanya, Mtima yeye hakuonekana kuwa na raha hata kidogo.
Roho ilikuwa inamuuma mno kuona watu wakihangaika kuokoa miili ya marehemu na wengine wakiwalilia. Alihisi kutenda dhambi isiyosameheka, mzimu wa ndoto aliyoiota ulizidi kumsumbua.
“Tuondoke,” alimwambia Abdulrahman.
“Sawa, inabidi twende mahali tukajipongeze kutokana na kazi tuliyoifanya.”
“Hapana, turudi mafichoni tukapumzike.”
“Kwa nini?”
“Basi tu nahisi siko vizuri.”
Abdulrahman hakuwa mbishi, walielekea kwenye gari lao na kuliondoa bila mtu yeyote kufahamu kuwa ndiyo walikuwa wahusika wa tukio hilo.
***
Kabla ya kuelekea Tanzania, Mtima na Abdulrahman walijifunza kupitia vitabu mbalimbali kikiwemo Tanzania Yetu, vilivyoeleza historia na habari mbalimbali za taifa hilo. Walichokigundua, nchi hiyo ilitawaliwa na amani sana. Hali iliyosababisha maeneo mengi kuwa na ulinzi duni. Hakukuwa na mashaka kabisa juu ya kutokea kwa uhalifu mahali popote pale.
Walichokifanya, waliyatafuta maeneo kwenye miji mikubwa ambayo walifikiri ikiwa watayasambaratisha wataliachia Taifa la Tanzania maafa makubwa, ambapo baada ya uchunguzi wao waliyapata maeneo yakiwemo Kituo cha Kibiashara cha Mlimani City, Dar, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jengo la Bunge, Dodoma, Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza na Hosptali ya KCMC, Moshi.
“Hapa twende wapi?” Abdulrahman alimuuliza Mtima.
“Dar es Salaam inatajwa sana, huko tutawashitua watu.”
Siku mbili baadaye walikuwa tayari jijini Dar es Salaam, wakajichimbia katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, kupitia vyombo vyao vya taarifa wakatangaza kufanya uhalifu wa kutisha katika eneo lolote maarufu.
Kutokana na jinsi walivyojifunza kuhusu Tanzania, waligundua hali ya serikali ya nchi hiyo kupuuzia mambo, ambapo walipofuatilia zaidi waligundua kuwa ulinzi ulidumishwa zaidi kwenye vituo vya kibiashara jambo lililowafanya waamue kwenda kufanya shambulio lao Muhimbili.
Shambulio hilo ndilo lililomuumiza sana moyo Mtima baada ya kushuhudia roho za watu wengi zikiteketea bila huruma yoyote ile, Mtima akakosa raha kabisa, alihisi macho ya watu wote duniani yakimtazama na kumlilia juu ya kile alichokuwa anakifanya, alijikuta akitamani hata kujitoa uhai.
“Una tatizo gani?” Abdulrahman alimuuliza Mtima baada ya kumuona hayuko katika hali ya kawaida.
“Kwani vipi?”
“Sikuelewi!”
“Huelewi nini?”
“Unaonekana una mawazo sana.”
“Hakuna kitu.”
“Kuwa mkweli kaka.”
“Ukweli upi unaoutaka?”
Mtima hakupenda kabisa kuwa muwazi kumwambia Abdulrahman juu ya sababu zilizomfanya akose raha, kila kitu alikifanya kuwa siri, jambo lililomshangaza zaidi rafiki yake huyo ni pale alipomwambia alihitaji muda zaidi wa kupumzika kabla ya kupanga tena kufanya shambulio lingine.
Kitendo hicho kilimfanya Abdulrahman kuhisi kuwa kuna jambo lilikuwa linaendelea akilini mwa Mtima ila hakupenda kumwambia, ikambidi kuwa makini na kufuatilia kwa ukaribu sana mwenendo za kijana huyo.
***
“Nimefikaje hapa?” Destiny aliuliza huku akijinyonganyonga kitandani. Lakini hakupata jibu, alipofumbua macho yake kwa shida alishangaa kuwaona watu wakiwa wamemzunguka huku wakilia kwa uchungu.
Hali hiyo ilizidi kumshangaza na kuichanganya akili yake maana hakuna alichokuwa anakikumbuka wala kumtambua mtu yeyote yule kati ya waliokuwa wamemzunguka.
Hali ya mshangao ikazidi kuongezeka baada ya kumuona mwanamke mweusi mwenye umri mkubwa akimshika kwenye paji la uso wake huku akimtamkia maneno ya kumtia moyo juu ya hali yake.
“Kuna nini?” aliuliza tena.
“Umeponea chupuchupu!”
“Chupuchupu! Kivipi?”
“Nitakwambia tu mwanangu kuwa mvumilivu.”
Je, nini kitaendelea? Destiny alifika vipi hospitali hata kukutana na mama yake? Vipi kuhusu Mtima? Usikose wiki ijayo.