
VIJANA walio kwenye mradi wa Jenga Kesho yako iliyo Bora (BBT) katika shamba la Chinangali leo Januari 27 wameungana na Watanzania wengine kumtakia heri na baraka Rais Samia Suluhu Hassan kwenye siku yake ya kuzaliwa.
Idadi kubwa ya vijana walikata na kula keki, kupata vinywaji kwa pamoja kisha kuimba nyimbo za kumbariki Rais Samia huku wakimshukuru kwa kuwasaidia kupata mashamba hayo.

Akizungumza kwa niaba ya vijana wa BBT, Katibu wa BBT- Chinangali, Innocent Zerote, amesema kuwa uamuzi wa Rais Samia wa kuwapatia mashamba na tena kuwaweka kwenye nyumba nzuri za kuishi umekuwa mkombozi kwa maisha yao.
“Leo tumeungana na Watanzania na watu wengine duniani kumtakia maisha mema Rais Samia kwa hakika kwetu huyu ni zaidi ya Rais hasa kutokana na alivyotufikia siye vijana kwa namba mbalimbali, tupo wa BBT lakini pia wapo wengine ambao wamefikiwa kutokana na sera nzuri za wizara ya kilimo, tumamtakia miaka 100 zaidi.” amesema Zerote.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde aliyekuwa kwenye ziara ya kikazi shambani hapo alijumuika na vijana hao kusherehekea siku hiyo ya kuzaliwa kwa Rais Samia na kutumia wasaha huo kuzungumza na vijana hao.
“Najua nilikuwa nimekuja kwa ajili ya shughuli za kikazi hapa shambani na nikakuta kumbe mna jambo lenu hili, sasa hapa na mimi ninapenda kuzungumza na ninyi hapa kama kaka yenu na siyo kama kiongozi, kwanza nawaomba sana hebu tambueni kuwa mtu yoyote anayefikiri kuwa maisha ni rahisi hawezi kufanikiwa” amesema Silinde.
Ametaka vijana hao kutambua kuwa BBT ilivyoanza siyo kama ilivyo sasa na kuwa hata kwa sasa hatua ilipofikia ni hatua nzuri inayowawezesha vijana hao kuanza kulima na kuwataka kufanya kazi kwa ufanisi ili kutimiza adhma ya Rais Samia ya kutoa ajira kwa vijana na kuendeleza kilimo.