
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeandika rekodi mpya ya ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2023/24 baada ya kufanikiwa kukusanya kiasi cha Tsh. Trilioni 27.64, ambayo ni sawa na ufanisi wa 97.67% ya lengo la kukusanya Tsh. Trilioni 28.30.
Taarifa ya Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi kupitia kwa Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidato imesema Makusanyo hayo ni ongezeko la 14.50% ikilinganishwa na makusanyo ya Tsh. Trilioni 24.14 katika Mwaka wa Fedha uliopita, 2022/23.
“Katika kipindi cha robo mwaka ya nne yaani Aprili – Juni, 2024, TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha Tsh. trilioni 7.09, sawa na ufanisi wa 99.46% ya lengo la kukusanya kiasi cha Tsh. trilioni 7.13, makusanyo haya ni ongezeko la 24% ukilinganisha na kiasi cha Tsh. trilioni 5.72 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha uliopita 2022/23” imesema taarifa hiyo.
