×

Simulizi za kusisimua… MKATABA – 5

ILIPOISHIA JUMATATU ..

Kwa mara ya kwanza Suma alijishangaa kugundua kitu cha ajabu sana. Pamoja na mapenzi yake yote juu ya viumbe hao, siku hiyo Suma alimuogopa!

“Nimekuuliza wewe ni nani?”

“Mimi ni jini Suma.”

“Jini?”

 

“Ndiyo…tena naamini nimekuja muda mwafaka. Nina mazungumzo kidogo na wewe kama kweli unapenda majini kama ninavyokuona ukihangaika,” akasema yule msichana aliyejitambulisha kuwa ni jini akiketi kitandani.

Suma akazidi kuogopa!

SASA ENDELEA…

HOFU iliutawala moyo wa Suma, alipata wakati mgumu kidogo wa kutafakari japo kwa sekunde tatu tu. Alitaka kujiridhisha kwamba aliyekuwa mbele yake alikuwa jini kweli au lah!

Lakini hata kama alikuwa jini kweli, bado alikuwa na mambo mengine ya kujiuliza.
Kwa nini awe mwoga leo kwa majini? Si ni yeye ndiye aliyeweka manukato makali na udi kwa ajili ya kuwaita?

“Ni nini hiki?” akajiuliza.
“Ni jini Suma,” yule msichana akamjibu.
Akashangazwa na kitu kingine kipya; yule msichana aliyesema ni jini alimjibu swali ambalo alijiuliza mwenyewe kichwani mwake, tena bila kutoa sauti.

Amesikiaje?

“Sawa tufanye ni jini, sasa kwa nini namuogopa?” akawaza tena.
“Hata mimi nakushangaa kwa hilo!” yule jini akamjibu.
Suma akatetemeka!

Kwa asilimia mia moja sasa aliamini aliyekuwa chumbani mwake alikuwa ni jini. Hilo hakuwa na shaka nalo hata kidogo. Ni kweli Suma alikuwa chumbani kwake.

Woga wake ukamfanya atake kurudi nyuma zaidi lakini haikuwezekana maana tayari alikuwa ameshafika ukutani.
“Suma!” yule jini akaita.
“Mmmmh!” Suma akaitika kwa kuguna.

“Napenda kusikia sauti yako, ingawa nimeshaisikia mara nyingi kabla.”
“Wewe ni nani kwani?” Suma akauliza baada ya kujikaza kidogo.
“Mimi ni jini.”

“Najua ni jini…unaitwa nani na unataka nini?”
“Suma acha hizo bwana, mimi nimekuja hapa kwa ajili yako maana wewe ndiye unayehitaji msaada wangu na si mimi kutaka msaada kutoka kwako. Kwa maneno mengine, ni sahihi zaidi mimi kuuliza nikusaidie nini?”

Suma akahema kwa kasi.
“Pole sana Suma.”
“Mh! Kazi ipo leo!” akawaza.
“Tena kubwa sana,” yule jini akamjibu.
“Sawa, sasa naanza kukuelewa lakini napenda kujua jina lako kama wewe unavyofahamu langu.”
“Naitwa Zukhaiya.”

“Zakhia?” akauliza kwa mshtuko kidogo.
Alimkumbuka Zakhia wake.
“Siyo Zakhia, nimesema Zukhaiya.”
“Sawa, kwanza umeingiaje humu ndani kwangu?”
“Achana na maswali ya kitoto. Twende kwenye hoja ya msingi, wewe si unataka kuoa jini?”

“Ndiyo.”
“Kwa nini jini na si binadamu?”
“Mambo mawili makubwa nahitaji; kwanza penzi la dhati lakini pia mali. Familia yangu ni duni sana.”
“Najua.”

“Nataka kuwasaidia wazazi wangu watoke kwenye umasikini, pia nami niishi maisha yasiyo na shida.”
“Umenena vyema.”
“Je, ni wewe?” Suma akauliza kwa shauku.
“Nani?”
“Nitakayekuoa?”

“Hapana.”
“Sasa kwa nini umekuja?”
“Nimesikia uhitaji wako. Nitakusaidia lakini kwa masharti.”
“Sawa, nipo tayari.”

Zukhaiya akasimama pale kitandani, akamwangalia Suma kwa macho yanayobadilikabadilika rangi kila baada ya muda mfupi. Akatabasamu kisha akainama kidogo na kuketi tena kitandani.
Ghafla akasogeza mdomo wake hadi ulipogusana na wa Suma.

Akamwangushia busu mwanana. Suma akashtuka. Zukhaiya akarudi nyuma kidogo kisha akambusu tena katika shavu la kushoto na baadaye la kulia.
Zukhaiya akamgeuzia mgongo Suma na kumtaka amfungue zipu ya gauni lake iliyokuwa mgongoni. Suma akashtuka!

“Lakini ulisema siyo wewe.”
“Nifungue zipu,” Zukhaiya akasema kwa sauti ya kuamrisha.
Suma akafanya hivyo.
“Nataka unifurahishe kimapenzi…” Zukhaiya akasema kwa sauti laini, harufu nzuri ikitawala katika chumba kile…
“Mh!”

“Tafadhali.”
“Sawa.”
Kazi kubwa ikafanyika. Kwa Suma kulikuwa na ugumu kidogo mwanzoni lakini baada ya muda akashangaa ametulia na kumzoea Zukhaiya. Zoezi hilo likakamilika kwa ukamilifu wake.
“Hapo sawa, umefanya vizuri sana.”
“Ahsante Zukhaiya.”

“Umemaliza jambo la kwanza…sasa tunaweza kufanya makubaliano.”
“Makubaliano gani tena?”
“Lazima tuingie mkataba.”
“Mkataba?”
“Ndiyo…mkataba tena wa siri.”
“Kwa nini siri?”

“Hutakiwi kumwambia mtu yeyote juu ya mkataba wetu. Mimi nipo hapa kama wakala.”
“Ni upi?”
“Nitakupa maelekezo, kwa sasa acha niondoke, kesho nitakuja tena,” akasema Zukhaiya akisimama na kuelekea mlangoni.

Suma akamwita lakini Zukhaiya hakugeuza shingo. Alitegemea kumuona Zukhaiya akifungua mlango na kuondoka lakini jambo hilo halikutokea…
Alitoweka!
Ilikuwa ghafla sana!
*

MBEZI BEACH, DAR
Uso wa Suma ulikuwa umechakazwa na machozi kama maji usoni mwake. Ustaadh Alii alimwangalia kwa huruma Suma. Alijua ni kwa namna gani kumbukumbu zile zilimtesa, hasa katika kipindi kigumu kama hiki ambacho anateseka kuliko kawaida.

“Suma jikaze, mimi na wenzangu tupo hapa kukusaidia. Sikia nikuambie, Allah hajawahi kushindwa hata siku moja. Kuwa huru, dua zetu zitajibu. Hebu niambie kilitokea nini baadaye?” Ustaadhi Alii akauliza.

“Acha tu Ustaadhi, sasa naanza kupata picha. Sijui kama naweza kuishi kwa amani tena.”
“Utaweza mwanangu, Allah anajua zaidi. Atakusaidia, tafadhali endelea kutueleza.”

“Basi baada ya hayo ya usiku ule, asubuhi nilikutana na kitu cha ajabu sana…” akasema Suma akiangalia juu, machozi yakishindwa kuacha kuuchafua uso wake.
*
Bado harufu ya mchanganyiko wa manukato iliendelea kupenye katika pua za Suma. Kwa kiasi fulani sasa alihisi kupaliwa! Akakohoa kwa nguvu kiasi kwamba alihisi mbavu zake zikichezacheza!
Akashtuka!

Moshi ulikuwa umejaa chumbani mwake lakini giza totoro nalo likichukua nafasi kubwa chumbani mwake. Jasho jingi lilikuwa likimtoka mwilini mwake.
Hapohapo akapata kumbukumbu mpya! Alimkumbuka Zukhaiya ambaye alikuwa naye chumbani hapo muda mfupi uliopita. Alisimama ghafla na kusogea mpaka mlangoni.
Mlango ulikuwa umefungwa!

Ni kweli muda mfupi uliopita alikuwa na jini aliyejitambulisha kwa jina la Zukhaiya, mara akamwambia anaondoka na alipofika mlangoni akatoweka ghafla.
“Mh!” akaguna Suma
“Alikuja kweli humu chumbani?” akawaza tena.

Suma akagundua kitu kipya. Pamoja na kwamba alikuwa akihisi kwamba alikuwa kwenye ndoto, sasa alianza kuwa na uhakika kuwa kweli jini Zukhaiya alikwenda chumbani mwake.
Alikuwa na dalili zote kuwa alikutana kimwili muda mfupi uliopita. Mazingira yote yalithibitisha hivyo.
“Kwahiyo nimefanya mapenzi na jini?” akawaza tena.

Taratibu akarudi kitandani na kuketi. Akakumbuka kitu. Alisimama haraka na kusogea kwenye swichi ya ukutani kisha akawaza taa. Akasogea kwenye meza ndogo ya kujipambia na kujitazama kwenye kioo.
Ndiyo…mashavu yake yote mawili yalikuwa na alama ya mdomo wa mwanamke aliyepaka rangi maalumu ya mdomo, wenyewe wanaita lip stick. Ni alama hiyo ndiyo iliyomthibitishia pasipo shaka kuwa kweli alikuwa na Zukhaiya ndani ya chumba chake.
Wazo lingine likauvamia moyo wake alikumbuka neno moja tu, kubwa na muhimu zaidi kwa muda wote aliozungumza na Zukhaiya;

MKATABA!
“Siyo mimi nitakayekuwa na wewe Suma, nipo hapa kuwawakilisha wenzangu lakini ni lazima tuingie mkataba,” akakumbuka maneno ya jini Zukhaiya.
“Mkataba?” swali hili aliliuliza yeye na alilikumbuka barabara.
“Ndiyo tena mkataba wa siri.”

“MKATABA?!!!” Akawaza sasa Suma.
“Ni mkataba gani sasa na alimaanisha nini aliposema tunatakiwa kuingia mkataba?” anazidi kuwaza.
Akiwa katika mawazo hayo, macho yake yakatua kwenye saa iliyokuwa ukutani. Mshale wa saa uligota kwenye mbili na wa sekunde ulikuwa umesimama kwenye 16.

Yes ilikuwa saa 8:16 usiku!
“Ni usiku sana saa hizi,” akawaza tena.
Aliutamani sana utajiri, lakini kwa mara ya kwanza alianza kuhisi kuwa na wasiwasi na uamuzi wake.

“Lakini bado nina nia ya kupata utajiri, sitakiwi kurudi nyuma katika wazo langu hili,” akawaza mwenyewe.
Ni muda huo ndipo alipoamua kuvuta shuka na kulala. Haikuwa kulala hasa kwa maana ya kulala bali alijilaza! Alisaka usingizi kwa muda mrefu sana lakini wapi!
Ataupata wapi?
Anamuwaza Zukhaiya.

 

Kusoma zaidi Simulizi za mwandishi, mfuate kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Facebook: Simulizi za Joseph Shaluwa Instagram: @josephshaluwa

ITAENDELEA IJUMAA

Leave a Comment