Mkurugenzi na mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Telegram, Pavel Durov amekamatwa jijini Paris, Ufaransa muda mfupi baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Paris-Le Bourget akitokea Arzebaijan akitumia ndege binafsi.
Msemaji wake, Georgy Loboushkin amewaambia waandishi wa habari kwamba Durov hakuwa na wasiwasi wowote kuhusu usalama wake ndiyo maana akaamua kwenda Ufaransa na kwamba anajua maagizo ya kukamatwa kwake yametoka Washington, Marekani.
Taarifa kutoka vyombo vya habari nchini Ufaransa zimeeleza kuwa mamlaka nchini humo zimemfungulia mashkata ya kusafirisha dawa za kulevya, kuwafanyia ukatili wa kingono watoto na utapeli, mashtaka ambayo yanawakabili watumiaji wa mtandao wake wa Telegram huku Durov akikataa kutoa ushirikiano kwa polisi kuhusu taarifa za wahalifu wanaotumia mtandao wake.
Inazidi kuelezwa kuwa amri ya kukamatwa kwa mtaalamu huyo wa teknolojia, raia wa Urusi inatajwa kutoka Marekani ambako FBI imekuwa ikimsaka kwa muda mrefu kwa tuhuma za kukataa kutoa ushirikiano kuhusu taarifa za watumiaji wa mtandao wa Telegram huku teknolojia kali ya kuzuia kudukuliwa kwa mtandao huo ikiufanya kuwa rafiki wa wahalifu wakubwa duniani.