
Kutokana na uharibifu wa mazingira uliokithiri nchini, wazazi na walimu wa shule za msingi na sekondari wametakiwa kuhakikisha kila mwanafunzi anayeanza elimu ya Msingi na sekondari anapanda mti na kuutunza mpaka anapomaliza elimu hiyo.
Maelekezo hayo yametolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango alipokuwa akiongea na wananchi katika kijiji cha Magiri wilayani Uyui mkoa wa Tabora.
Aidha kutokana na mkoa wa Tabora kupoteza hekta 7000 za miti kutokana na uanzishwaji wa mashamba mapya na ukataji wa miti kwaajili ya kutumika kwenye kukausha tumbaku, makampuni ya ununuzi wa tumbaku yametakiwa kuchangia shughuli za upandaji miti ili kutunza mazingira na kuwezesha kurudisha uoto wa asili unaoharibiwa kwa kukata miti.

Vilevile Naibu Waziri wa Maliasili, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) ambaye naye ameambatana na Makamu wa Rais katika ziara hiyo alisema kuwa Wakala wa Huduma za misitu Tanzania (TFS) kwa mwaka huu wa fedha imepanga kuzalisha miche milioni 1 ya miti kwa ajili ya kusambaza kwa wananchi na taasisi mbalimbali katika mkoa wa Tabora.
Katika hatua nyingine Mhe. Kitandula aliwahamasisha wananchi wa mkoa wa Tabora kuchangamkia fursa kubwa ya soko la mazao ya Nyuki nchini China kufuatia Serikali za Tanzania na China kusaini hati ya makubaliano kwa Asali ya Tanzania na mazao mengine ya Nyuki kuuzwa nchini China.

Vilevile aliwakumbusha wananchi wa Tabora kuwa mwaka 2027 Tanzania itakuwa Mwenyeji wa Mkutano mkubwa wa wadau wa mazao ya ufugaji Nyuki Duniani, hivyo huu ni wakati mzuri wa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye mazao yatokanayo na ufugaji wa nyuki kisasa na wenye tija, hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa inayozalisha asali kwa wingi kutokana na misitu iliyopo.
Mhe. Makamu wa Rais, yupo kwenye ziara mkoani Tabora kwa ajili ya kuangalia na kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita. Katika ziara hiyo Naibu Waziri wa Maliasili na utalii anashiriki akiwa ameongozana na wataalamu kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA)