×

Waziri Mkuu Amwakilisha Rais Samia kuaga mwili wa marehemu John Billy Tendwa Viwanja vya Karimjee

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Desemba 19, 2024 amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kuaga mwili wa marehemu John Billy Tendwa ambaye aliwahi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Akitoa Salama pole kwa waombolezaji wakati wa tukio la kuaga lililofanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa wanafamilia, ndugu na waombolezaji kuyaenzi mema yote aliyoyafanya marehemu Tendwa katika kipindi cha uhai wake.

Amesema kuwa Marehemu Tendwa alikuwa mtumishi wa umma ambaye mara zote alitekeleza majukumu yake kwa weledi, ujasiri na uadilifu mkubwa katika kipindi ambacho vyama vya siasa vilikuwa vinajijenga. “Tunaungana na wanafamilia katika kuomboleza msiba huu, sote tuna jukumu la kuombea na kuenzi kwa kuyaendeleza mazuri yote aliyoyafanya katika nchi hii”

Naye, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Marehemu Tendwa alikuwa na sifa ya ukweli kwa vyama vyote vya siasa, ujasiri na kutokuwa na upendeleo. “Kwa Kiasi kikubwa amesaidia kujenga demokrasia ya vyama vingi nchini na huwezi kuzungumza kuhusu ustawi wa vyama vya siasa nchini bila kumtaja Marehemu Tendwa”

Kwa Upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi amesema kuwa kifo cha Marehemu Tendwa si pigo kwa familia tu bali kwa wale wote wanaotambua thamani ya mchango wake katika siasa ya demokrasia ya vyama vingi nchini.

Marehemu Mzee Tendwa alihudumu katika nafasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kipindi cha miaka 12 kutoka Mwezi Mei 2001 hadi Agosti 2013. Marehemu Mzee Tendwa alifariki Desemba 17, 2024 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.

Baadhi ya viongozi walioshiki kuaga mwili wa Marehemu Mzee Tendwa ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderianaga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonaz.

Leave a Comment