
JESHI nchini Guinea ambalo limeshika madaraka nchini Guinea limetangaza kuwa Rais aliyeondolewa madarakani nchini humo, Alpha Condé (83) ameachiwa kutoka kizuizini na kupelekwa nyumbani kwa Mkewe katika mji mkuu Conakry.
Katika taarifa yake iliyotangazwa kwenye televisheni ya Serikali Jeshi limesema Condé sasa yuko na Mkewe, Hadja Djene Kaba Condé na kusisitiza kuwa Jeshi litaendelea kumpatia Rais huyo wa zamani heshima anayostahili bila shinikizo la kitaifa au kimataifa.
Alikuwa ameiongoza Guinea tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2010, katika makabidhiano ya kwanza ya mamlaka ya kidemokrasia nchini Guinea.
Guinea ilisimamishwa kutoka muungano wa kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, kufuatia mapinduzi hayo.
ECOWAS pia iliweka marufuku ya kusafiri na kufungia mali ya viongozi wa mapinduzi ya Guinea na familia zao huku ikitaka Bw Condé aachiliwe bila masharti.