
Sasa ni rasmi adhabu ya kifo imeondolewa nchini Zimbabwe baada ya Rais wa nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa kutia saini sheria inayoondoa adhabu hiyo katika taifa hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya bunge la Zimbabwe kupiga kura mapema Desemba kufuta hukumu ya kifo katika taifa hilo.
Rais Mnangagwa amekuwa mkosoaji wa muda mrefu wa adhabu ya kifo, akitaja kuhukumiwa yeye mwenyewe hukumu ya kifo katika miaka ya 1960 kwa kulipua treni wakati wa vita vya msituni vya kudai uhuru.
Hukumu ya kifo iliwekwa katika nchi hiyo wakati wa utawala wa kikoloni wa Uingereza.
Zimbabwe ilitekeleza hukumu ya kifo ya kunyonga kwa mara ya mwisho mwaka 2005, japokuwa mahakama zake ziliendelea kutoa hukumu ya kifo kwa makosa makubwa kama vile mauaji.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limepongeza uamuzi huo na kusema ni dalili ya matumaini kwa watu wanaotaka kukomeshwa hukumu ya kifo katika eneo hilo, lakini limeonyesha masikitiko yake kwa tarifa kwamba hukumu ya kifo inaweza kurejeshwa wakati wa hali ya hatari.
Lakini Amnesty imeitaka serikali ya Zimbabwe kuondoa kifungu kinachoruhusu matumizi ya hukumu ya kifo wakati wa hali yoyote ya hatari.
Kulingana na Amnesty, kuna nchi 113 duniani, zikiwemo 24 kutoka barani Afrika ambazo zimeondoa kikamilifu hukumu ya kifo, na kubainisha kuwa nchi tano zilizo na idadi kubwa ya watu walionyongwa mwaka 2023 ni China, Iran, Saudi Arabia, Somalia na Marekani.
Stori na Elvan Stambuli | GPL