×

Penzi Kabla y a Kifo-19

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Msichana mwenye mafanikio na bilionea, Elizabeth Marcel anamuona mtoto mgonjwa hospitali ya Muhimbili. Moyo wake unaguswa na kujikuta akiwa na hamu ya kumsaidia mtoto huyo. Hivyo anaanza kumfuatilia.SONGA NAYO…

Huruma ilimjaa moyoni mwake, kitu pekee alichotaka kufanya ni kumsaidia mtoto Glory aliyekuwa hoi kitandani. Kwa sababu nesi yule alikuwa akiendelea kumhudumia Glory, wakamsubiri mpaka atakapomaliza ndipo waende kwa daktari yule.

Kila alipomwangalia Glory, hakuacha kulia, maumivu makali ya moyo yalimkamata na kujiona akishindwa kabisa hata kumwangalia, alichowaambia Candy ni kutoka na kusogea pembeni, wakafanya hivyo.

Baada ya nesi kumaliza kumhudumia mtoto yule, akawachukua na kumpeleka katika ofisi ya daktari aliyehusika katika suala zima la wagonjwa waliokuwa katika Wodi ya Mwaisela. Walipofika, wakaanza kuelezea shida yao ambapo hapohapo daktari akaonesha sura iliyokuwa na tabasamu pana.
“Tumekubaliana na msaada wenu, hakika tumehangaika sana,” alisema daktari yule.

Kuhusu fedha halikuwa tatizo, alichokifanya Elizabeth ni kuaga na kuahidi kurudi tena kesho yake kwa ajili ya kutoa kiasi hicho ili safari ya kuelekea nchini India ianze.

Alipofika nyumbani kwake, akajifungia chumbani na kuanza kulia kwa uchungu.
Alikuwa na maumivu makali mno ya moyo, kila alipokaa na sura ya Glory kumjia kichwani mwake, akajikuta akilia kwa uchungu kwani hakuamini kama kulikuwa na binti mdogo aliyekuwa kwenye mateso makali kama alivyokuwa Glory.

Siku iliyofuata, asubuhi na mapema akaondoka na kuelekea hospitali. Hakutaka kuacha kuvaa baibui na nikabu usoni. Hakutaka kuleta usumbufu wowote ule ndiyo maana hata gari alilokuwa akilitumia ni lile ambalo halikuzoeleka kabisa.

Alipitia benki ambapo alichukua kiasi cha shilingi milioni kumi na kuelekea huko. Alipofika hospitali, moja kwa moja wakaenda kwa daktari yule na kumuona kwa ajili ya kumwambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari na ni safari ya kuelekea India ndiyo iliyotakiwa kufanyika mahali hapo.
“Kiasi cha fedha hiki hapa,” alisema Elizabeth huku akiweka bahasha kubwa ya kaki mezani, ndani yake zilijaa noti.

“Kiasi gani?”
“Milioni kumi. Si zitatosha?”
“Ndiyo! Basi subiri tukuitie ndugu yake. Tulimwambia kuhusu suala lako, alilia sana kwa furaha, hakuamini kama mwisho wa siku ndugu yake angeweza kupata msaada,” alisema daktari.
“Hakuna tatizo.”

Alichokifanya ni kunyanyua simu na kupiga upande wa pili, baada ya sekunde kadhaa simu ikapokelewa na mtu wa upande wa pili na sauti laini ya kike ikaanza kusikika. Alichoagiza daktari huyo ni ndugu wa Glory apelekwe ofisini kwake kwa ajili ya kukutana na mdhamini aliyejitolea kumsaidia mdogo wake.
“Hakuna tatizo!” sauti ya upande wa pili ilisema na kisha simu kukatwa.

Walikaa na kuzungumza mengi, Elizabeth hakuacha kumwambia daktari jinsi alivyojisikia juu ya hali aliyokuwa nayo Glory, alionekana kuwa miongoni mwa watu waliomuonea huruma binti yule mdogo na hivyo daktari kumtakia baraka nyingi pasipo kugundua kwamba mtu aliyekuwa akizungumza naye alikuwa Elizabeth, msichana mwenye fedha na umaarufu mkubwa.

Baada ya dakika kumi, mlango ukaanza kugongwa, daktari akaruhusu waingie, nesi mmoja alitangulizana na kijana mmoja aliyeonekana kupigwa sana na maisha, Elizabeth alipoyageuza macho yake na kumwangalia kijana huyo, akausikia moyo wake ukipiga paa.
Elizabeth akachanganyikiwa, hakuamini kile alichokiona, kijana aliyesimama mbele yake, James alikuwa mzuri wa sura, mapigo ya moyo wake hayakutulia, yaliendelea kudunda kwa nguvu kana kwamba moyo ulitaka kuchomoka.

Mapenzi ya ghafla yakamkamata, yakampelekesha na kujikuta akiwa hoi, pasipo kulazimishwa na mtu yeyote yule, akajikuta akiingiwa na ugonjwa wa kupendapenda, akajikuta akianza kumpenda kijana yule maskini asiyekuwa na kitu chochote.

Candy alilifahamu hilo, alimjua vilivyo rafiki yake huyo, kila alipomuona mwanaume mzuri wa sura, alichanganyikiwa na kujikuta akitaka kuwa naye, alipomuona James, jinsi alivyokuwa mzuri alijua fika kwamba hata rafiki yake angempenda vilivyo. Hapohapo Elizabeth akavua nikabu, kila mmoja akashtuka.

“Ninahitaji nimsaidie mdogo wako ni binti mzuri ambaye hastahili kuwa kwenye mateso makali namna ile,” alisema Elizabeth huku akimwangalia James.

“Nashukuru sana Elizabeth, sina cha kukulipa, nashukuru sana.”
“Usijali! Usinishukuru mimi, mshukuru Mungu ambaye amefanikisha mimi kukutana na mdogo wako,” alisema Elizabeth, hakutaka kujiweka juu, kila siku alikuwa mtu wa kujishusha tu.

Je, nini kitaendela? Fuatilia wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave a Comment