
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA-Bara, Amani Golugwa leo amefika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kufuatia wito wa Polisi uliotolewa kwake na Jeshi hilo Februari 24, 2025.
Mhe Golugwa alisindikizwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Bara, John Heche, Mjumbe wa Kamati Kuu Mhe Godbless Lema na Wakili wa Kujitegemea Hekima Mwasipu

Baada ya kufika ofisini Kamanda wa Upelelezi wa Mkoa Davis Msangi – SSP alimweleza Golugwa atoe ufafanuzi wa kitu gani kimepangwa kufanyika tarehe 27/02/2025 kupitia kauli ambayo amesikika kwenye video fupi jongefu akizungumza katika kuhamasisha kuhusiana na tukio la kichama linalokusidiwa kufanyika tarehe hiyo.
Kamanda SSP Msangi aliipokea taarifa na maelezo yalitolewa. Aidha, viongozi wa chama walionyesha masikitiko yao kwamba jambo hili halikuhitaji usumbufu wa namna hii, bado ingekuwa rahisi tu kwa jeshi la polisi kupiga simu na wangeweza kupata taarifa na maelezo ambayo yangetosheleza.
Tarehe 27/02/2025, chama kinakwenda kuzindua tukio kubwa la kuwaunganisha Wanachama na Watanzania ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu harakati za mabadiliko nchini.