×

UN yatiwa wasiwasi na hali tete Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema anasikitishwa sana na kuendelea kushtadi taharuki na hali ya mambo nchini Sudan Kusini.

Kupitia msemaji wake, Stephane Dujarric, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya jana kwamba, nchi hiyo ya Kiafrika ipo katika hali tete ma hatari ya  kutumbukia tena kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kauli hiyo imekuja kufuatia ripoti za kuwekwa kwenye kifungo cha nyumbani Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar katika mji mkuu, Juba.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) unatoa wito kwa pande zote nchini humo “kujizuia na kuzingatia Mkataba Uliohuishwa wa Amani (RPA),” amesema. Dujarric na ameongeza kuwa: Ujumbe wa kulinda amani unaungana na washirika wengine wa amani wa kikanda na kimataifa katika kuelezea wasiwasi juu ya kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwa Machar.

Kadhalika Katibu Mkuu wa UN kupitia msemaji wake amezitaka pande zote kuheshimu makubaliano ya mwaka 2018 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Mvutano kati ya vikosi vinavyomuunga mkono na Rais Salva Kiir na vile vya Makamu wa Rais, Riek Machar (pichani) unaendelea kutokota

Kufuatia taarifa hiyo ya kukamatwa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini na vyombo vya dola, Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Nicholas Haysom alisema, pande zote zinapaswa kujizuia na kudumisha Mkataba wa Amani Uliohuishwa.

STORI: ELVAN STAMBULI