ILIPOISHIA
Kama vile hiyo haitoshi, nilimchukua ndege na kumuweka kwenye kopo na wote wakashuhudia nikilipondaponda lile kopo lakini nilipofunua kapu dogo lenye kuzibwa juu ili ndege asiruke alikutwa mle akiwa hai. Watu walipigwa na butwaa na kusema mimi ni nabii kweli na kwamba nikitupwa kwenye shimo la kifo, nchi itatikisika.
Mfalme alisimama akautazama umati uliokuwa ukinishangaa huku wengine wakisema mimi siyo mtu wa kawaida.
“Sikilizeni,” akaanza kuhutubia mfalme na watu wote wakawa kimyaa ili kumsikiliza.
“Katika maisha yangu sijaona mambo ya ajabu kama haya.
SONGA NAYO…
“Haya ni mambo ya ajabu sana lakini hatuna la kufanya, sheria yetu ni kwamba mtu akiharibu mazingira, yaani kukata mianzi tena michanga ni lazima atupwe kwenye shimo la kifo.”
“Maulana, kama utatutupa kwenye shimo la kifo tukafa wote hakika nakuambia kuna jambo zito sana litatokea katika nchi hii ambalo hutalisahau,” niliamua kumtisha kwa sababu nilijua tayari nina hukumu yangu, hivyo bora nimtishe ili akitaka atuachie au lolote na liwe.
Watu wakapigwa na butwaa kuona nina ujasiri wa kumpasulia hayo mkuu wa nchi lakini walikuwa kimyaa kusikiliza uamuzi wa kiongozi huyo.
“Bwana Issa Namakoto pamoja na maajabu haya uliyotuonesha pamoja na maneno yako mazuri na yale ya vitisho, sheria haikuachi nayo ni msumeno, utatupwa kwenye shimo la kifo. Kama maajabu basi utayafanya humohumo shimoni,” watu wengine wakawa wananong’onezana maneno ambayo sikuweza kusikia.
Niliwekwa pembeni kusubiri adhabu yangu kisha akafuata msichana ambaye wote tulikuwa tunajua kuwa alikuwa mjamzito japokuwa mimba yake ilikuwa changa na ilikuwa haijaanza kujitokeza.
Alikuwa wa kwanza kuitwa kwa upande wa wasichana. Yule Kamanda Ben Mtwanga alichukua karatasi yake aliyoandika majina yetu akasoma kwa sauti:
“Maimuna Mpepechere! Sogea kwa mkuu wa nchi.”
Nilimuona msichana huyo akiisogelea meza ya kiongozi wao huku mwili ukitetemeka kama nilivyosema awali. Mara baada ya kufika mbele yake akaambiwa na mkuu huyo:
“Mimi naitwa Maimuna Mpepechere…” alisema msichana huyo huku akitetemeka kama kifaranga kilichotumbukia kwenye maji.
“Kama nilivyompa nafasi kiongozi wenu, hii nawe ni nafasi yako ya kujitetea nione kama nitakusamehe au nawe siku yako duniani itaishia leo. Nakusikiliza anza utetezi wako.”
“Utetezi wangu mtukufu kiongozi ni kwamba nina mimba ya miezi miwili na nimemuacha mchumba nyumbani tulipotoka.”
Mfalme alimuangalia yule msichana kisha akasema:
“Maimuna Mpepechere wewe hutatupwa shimoni. Utakuwa katika uangalizi maalum ili kuthibitisha madai yako. Nakupa onyo, kama utakuwa unadanganya, utakatwa kichwa.”
“Sidanganyi mfalme ni kweli tupu,” Maimuna alijitetea.
“Haya ukweli tutaubaini siku zijazo kwani mimba tumbo huwa linatoka mbele na kamwe haliingii ndani. Mjamzito kisheria hawezi kuuawa,” alisema kiongozi wa nchi.
Yeye alipelekwa upande mwingine tofauti na nilipowekwa mimi.
Akafuata kijana wa kiume aitwaye Alex Kwiimukaga.
Baada ya kuitwa jina lake nilimshuhudia akienda mbele ya kiongozi huyo mkuu.
“Kijana hii ni nafasi muhimu kwako, jitetee.”
Nilimuona kijana Kwiimukaga akishindwa kutoa neno kutokana na hofu aliyokuwanayo.
Baada ya muda kidogo tulishuhudia suruali yake ikiloa kwenye zipu, baadaye majimaji yakaendelea kuteremka hadi chini, nikagundua kuwa alikuwa anajikojolea kutokana na kuingiwa na woga baada ya kuonana ana kwa ana na kiongozi huyo wa nchi huku akiwa hana la kujitetea.
Alex Kwiimukaga ambaye tulizoea kumuita Kwiimuka ndiye alikuwa kiongozi wa ukataji wa mianzi kule kwenye bustani ya Nangose.
Kijana huyo nguvu za kutoka pale kwa mkuu zilimuishia ilibidi abebwe na askari na aliketishwa nyuma yangu.
Alifuata dereva wetu wa mini basi, Bwana Limbende. Baada ya jina lake kuitwa alikwenda mbele ya mfalme bila woga.
“Bwana Limbende, jitetee?”
“Mtukufu kiongozi mkuu. Mimi nilikuwa dereva tu wala siyo mtu wa ziara ya kutembelea Bustani ya Nangose. Nisingekodiwa nisingefika sehemu ile tukufu. Hivyo mtukufu nakuomba uniachie.”
“Ina maana wewe hukuja pale kutalii yaani kuiona ile Bustani ya Nangose?”
“Haswa mfalme. Tena basi nilikuwa naelekezwa njia maana sikuwahi kufika hata siku moja.”
Nilimuona mfalme akitikisa kichwa kukubali maelezo yake.
Aliitwa mtunza bustani, mzee Mavaka na kuulizwa kama alichokuwa akisema dereva Limbende ni kweli.
“Mtukufu alichokisema huyu bwana Limbende ni kweli kwa sababu yeye hakushuka kabisa kwenye basi lake wakati vijana hawa wanafanya uharibifu wa mianzi.
“Tena basi alikuwa akiwasihi wasiiharibu lakini vijana hawa wakawa wanampuuza, mzee Mavaka alizidi kumtetea.
“Wewe bwana Limbende, hutatupwa kwenye shimo la moto. Uko huru, askari mpeleke pale alipo msichana aliyedai ni mjamzito.”
Alichukuliwa na askari na kuwekwa kwenye hema moja na yule msichana mwenye mimba, Maimuna Mpepechere.
Baadaye alifuata utingo wake ambaye naye alisamehewa kwani alijieleza kama dereva.
Zoezi hilo liliendelea kwa wenzangu wote kuhojiwa mmoja baada ya mwingine na kiongozi huyo na kujikuta wengi wakihukumiwa kutupwa shimoni.
Aliyesalimika katika kundi letu ni yule msichana mjamzito, dereva na utingo wake ambao walipelekwa kukaa nyuma ya jukwaa la kiongozi yule lakini hawakuwa na raha kutokana na kujua kuwa sisi wenzao tunakwenda kutupwa kwenye shimo la kifo.
Wasichana waliohukumiwa pamoja nasi wanaume walikuwa wakilia kwa kwikwi.
Tuliamriwa kusimama na kuanza safari kuelekea kwenye shimo ambalo liliandaliwa kwa shughuli hiyo.
Yule msichana aliyekuwa mjamzito alikuwa akilia kwa sauti huku akipunga mikono ishara ya kutuaga.
Kilio chake kilifanya hata sisi wanaume tuanze kulia, mimi huwa mgumu sana kulia lakini yowe za yule dada zilinifanya nitokwe na machozi.
Je, kilijiri nini? Fuatili wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.