ASSALAM alaikum wapendwa wasomaji wa safu hii maridhawa, ambayo ni mwanana, inayokuelimisha na kukumbusha kila kukicha. Wapo baadhi yetu hujikuta wamesahau wajibu wao au wanajifanya wamesahau, sasa hapa ndipo haswaa mahala pake.
Katika pitapita yangu uswahilini siku moja asubuhi, nilifanikiwa kukutana na akina mama kama watatu, kila mmoja kwa wakati wake wakiwa wamevaa kanga moja wakipishana na wanaume, ambao baadhi yao ni waume za watu.
Mbaya zaidi wanawake hao pia wana waume zao lakini wamewaacha vyumbani, wao wanatoka tena wakiwa na miswaki mikononi.
Hivi mwanamke mwenzangu nikuulize, sasa ni kwa nini unamvalia jirani yako kanga moja? Hujui unajiaibisha? Hujui unamchoresha mwenza wako? Kwa nini mnafanya hivyo ni kweli hamjui madhara au mnatafuta soko? Jiwekeni hadharani basi watu wajue badala ya matangazo ya kimyakimya.
Sasa niwaeleze tu sababu ya kuandika hili, nilijikuta napata aibu baada ya mama fulani kutoka na kikanga chake nje ya nyumba, bahati mbaya akajikwaa, akaanguka tena mbele ya jirani wa kiume nikiwa nashuhudia, nikwambie alikuwa amevaa nini huko ndani? Akha mwenzangu, hata kufuli hakuwa nalo, nikamuinua kwa aibu, nikakimbilia ndani kwangu!
Siku iliyofuata nilimhoji, akadai alibanwa sana na haja ndogo ndiyo maana alitoka haraka. Hivi wanawake wenzangu niwahoji, hamjui maana ya nguo ya usiku au nguo ya kulalia? Kwa nini usiiandae nguo yako kwa mambo kama hayo, unajiaibisha kwa nini mke wa mtu?
Nguo ya kulalia haina maana ukapande nayo kitandani, maana yake ni kwa dharura kama hizo, lakini pia kanga au kitenge kuwa pembeni ni muhimu sana kwani huwezi kutoka na nguo ya usiku bila kujitanda kwa sababu nyingine huwa zinaonesha maumbile.
Wanawake mnaowafanyia hivyo majirani zenu mjue hamuwezi kuishi salama na jirani yako wa kike, kwa sababu atajua unatafuta mbinu za kumtega mumewe hivyo kuleta migogoro isiyo na sababu. Hivyo nawasihi mbadilike kwani mnawaweka wenzenu mioyo juu na nyie mnahatarisha amani yetu.