Ilipoishia wiki iliyopita
“Sasa dada Mwani tukusikilize ili utueleze jinsi gani huu mchezo unavyoweza kufanyika na kutuwezesha kufikia malengo bila kuacha alama nyuma yetu,” Bata alianzisha mazungumzo huku wasichana hao watatu wakionekana kuwa tayari kwa lolote.
Sasa endelea
Mwani akakohoa, ishara ya kujiweka vizuri kabla ya kuzungumza, kila mmoja naye akajiweka tayari kwa kusikiliza, Jully ambaye alikuwa amechomeka headphone katika masikio yake, akaichomoa. Wakatazamana, wote wakaachia tabasabu la shauku.
“Ile nyumba wanayokaa hao watu mimi naifahamu vizuri sana, enzi zile za utoto tukisoma, rafiki zangu ambao sasa hivi wako Ulaya, ile ndo nyumba yao. So naujua kila uchochoro. Wakati f’lani tulikuwa tunacheza michezo ile ya kujificha, kuna chemba moja ya maji machafu inatoka nje hadi kwenye korongo lipo kwa nyuma.
“Ni kiasi cha kwenda kuliangalia upya, mtu akipenya mle anatokea kwenye kichochoro f’lani hivi nyuma ya jiko ndani ya nyumba. Sidhani kama wamefanya marekebisho yoyote ingawa wale marafiki zetu wana miaka kama mitano hivi tangu baba yao aende Ulaya kikazi,” Mwani alianza kuwapa habari wenzake, ambao walionesha shauku kubwa.
Akawasimulia pia mazingira ya ile nyumba jinsi inavyoweza kuingilika kirahisi, lakini akagusia hata siku moja, yule dereva wa teksi inayowachukua wale watu mara kwa mara, aliwahi kumtongoza, hivyo kama itapendeza, anaweza kujitongozesha upya ili kupata habari mpya zaidi za mle ndani.
Mwishoni, wakakubaliana kuwa waanze kufanya uchunguzi wa ile chemba kama inaweza kuwa bado haina kizuizi cha kuingilika, kabla ya kufikiria kumtumia Mwani kujitongozesha kwa Sule, kwa sababu kwa vyovyote jambo hilo lazima limalizwe haraka.
Ni katika kikao chao hicho Mwani alipowaambia kuwa watu wale wanahisiwa kufanya biashara isiyo halali ingawa haifahamiki, kwa sababu wamekuwa na maisha ya siri mno, jambo linalowapa wasiwasi majirani zao.
Walipomaliza mazungumzo muhimu na mbuzi wao alikuwa tayari, wakaletewa mezani, wakamshambulia kwa zamu kabla ya kujichanganya kwa vinywaji na muziki hadi usiku mnene walipotafuta usafiri na kurejea nyumbani kwa akina Bata ambako wote walilala!
***
“Niambie mzee,” Sule alimwambia Twaha baada ya kuwa wamesalimiana na wote wakiwa na vinywaji vyao, maana Twaha naye alikuwa mtu wa bia.
“Hamna mpya ndugu yangu, tunasikilizia majipu tu, maana yanatumbuka kila siku, Magufuli kweli kiboko,” Twaha alijibu na kumfanya Sule kumuunga mkono, wakikubaliana kweli Tanzania imempata kiongozi iliyokuwa ikimsubiri kwa muda mrefu.
Baada ya mazungumzo ya kisiasa na kijamii kwa muda wa kama dakika 20 hivi, ndipo Sule alipoamua kumweleza mwenzake sababu hasa ya kumuomba wakutane.
“Nina mshkaji wangu anaitwa Jerry, jana nilimwambia nitakuwa mitaa hii maana kuna ishu nitaifuatilia, sasa kwa sababu yeye ni mwenyeji mitaa hii, nikamwomba kama anaweza akanionesha kiwanja tulivu huku na kama hata kuna mshkaji wa kupiga naye stori maana mimi siyo mtu wa mademu, ndiyo akanipa namba hii akasema wewe ni mwanae unakaa mitaa hii na akanielekeza hapa Johannesburg,” Sule alianza porojo zisizo na chembe ya ukweli.
“Jerry yule mshkaji wa South?” Twaha alimkumbuka Jerry, maana siku tatu zilizopita walikuwa pamoja eneo hilo.
“Yaaa, ndiye huyo huyo,” Sule alimkubalia na tangu wakati huo, vinywaji vikaanza kumiminika na mazungumzo yakakolea, kiasi cha mtu asiyewafahamu, kudhani kuwa ni washkaji wa zaidi ya miaka 30.
Sule alijitahidi sana kubadilisha mazungumzo kila baada ya dakika ishirini, kiasi kwamba hadi ilipofika saa mbili za usiku, tayari walishaongea kuhusu siasa, michezo, ugaidi, biashara ya unga, ukahaba, mashoga, ufisadi, bunge na hata uchaguzi wa Marekani.
Lakini katika mazungumzo yote hayo, hakukuwa na dalili za Twaha kurejea maelezo yake ya siku tatu zilizopita ili Sule ajue sehemu ya kuanzia. Lakini kwa kuwa alishampata na kumfahamu mtu huyo, ilipofika saa nne usiku, Sule aliaga, akisingizia mtu aliyemfuata amepata udhuru, hivyo atamtafuta siku nyingine, lakini wakiwa tayari wameshatengeneza urafiki wa karibu.
***
Mwani alikuwa kwenye korongo lililo umbali wa mtupo wa jiwe kutoka nyumbani kwao, eneo ambalo kwa zaidi ya miaka kumi hakuwahi kufika. Akiwa amevaa kaptura ya jinzi nyeusi na kitopu cheusi pia, alienda na kukaa chini ya mti ambao chemba iliyotoka kwenye nyumba ya akina Jerry inatokea.
Baada ya kujihakikishia usalama wa kutosha, akainuka na kuanza kuichunguza vizuri.