Na Imelda mtema, Risasi Jumamosi
MNENGUAJI wa kitambo Bongo, Maria Soloma anayeitumikia Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ amesema kuwa hatarajii kuachana na kazi ya unenguaji mpaka ‘anashika mkongojo’ kwani ni kazi ambayo haina madhara kwake.
Mnenguaji huyo aliyetumikia bendi tofauti nchini kabla ya kurejea kwa mara nyingine Twanga, amezungumzia mambo mengi katika mahojiano maalum na mwanahabari wetu:
CHANGAMOTO
“Kwa kweli changamoto ninazozipitia ni kwamba watu wengi wanaidharau kazi ninayofanya wanaichukulia tofauti kabisa kumbe ni kazi kama zilivyo nyingine na kuna wakati mtu anakuja kukutunza ukiwa unacheza jukwaani anataka kukuwekea hela kwenye maziwa au makalio kitu ambacho siyo kizuri kwa kuwa kuna wakati wanakuja wachumba zetu na hata wazazi na ndugu ambao tunaheshimiana, inaleta picha mbaya.
KUHUSU FAMILIA NA KAZI YAKE!
“Kwanza kabisa mimi nina mzazi mmoja tu ambaye ni mama, baba alishatangulia mbele ya haki lakini mama yangu pamoja na ndugu zangu wengine wanaithamini kazi yangu kama ilivyo kazi wanazofanya watu wengine na tena wao ni wapenzi wakubwa wa Bendi ya Twanga Pepeta ninayoitumikia.
KUHUSU MPENZI WAKE NA KAZI YAKE
“Hakuna kitu kizuri kama mtu akikuelewa kabla hata hajakufuata na kuanza mapenzi, mimi mtu wangu anajua kazi yangu vilivyo na mara kwa mara haachi kuja ninapocheza na ananisubiri tunapomaliza tunaondoka pamoja kwenda nyumbani.
KUACHANA NA UNENGUAJI
“Sijawaza wala kufikiria kabisa kuachana na hii kazi kwa sababu hakuna kitu kizuri kama kufanya kazi ambayo unaipenda kwa moyo mmoja. Siiachi kazi hii mpaka nashika mkongojo.
KUHUSU WATOTO
“Nina mtoto mmoja wa kike ambaye kwa sasa yupo kidato cha kwanza ambaye nilizaa na mwanamuziki Muumini Mwinjuma na hata bado sijafikiria kupata mtoto mwingine kabisa kwa sasa.
MAFANIKIO
“Faida ni nyingi sana, kwanza nimeweza kwenda nchi mbalimbali kwa ajili ya unenguaji na pia nimeweza kujikimu kimaisha maana bila hii kazi, maisha yangekuwa magumu sana.
KUIHAMA TWANGA
“Hapana kwa hivi sasa sifikirii kabisa kuhamia bendi yoyote hapa nimefika,” anasema Maria.