
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 17, 2025 ametoa wito mahsusi kwa vijana wa Tanzania kuamka na kuchukua nafasi yao katika kujadili na kushiriki kwa dhati ajenda za maendeleo ya taifa, akibainisha kuwa ari hiyo imeanza kudorora katika jamii.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Rais Samia amesema kuna haja ya kurejesha utamaduni wa mijadala ya maendeleo, hasa miongoni mwa vijana ambao ndio msingi wa taifa la kesho.
“Mtakubaliana nami kwamba kuna hali ya kudorora kwa ari ya kujadili masuala ya maendeleo katika jamii yetu, hususan miongoni mwa vijana ambao ndiyo tegemeo letu katika kujenga kesho iliyo bora. Hii siyo sawa hata kidogo,” alisema Rais Samia.
Amesisitiza kuwa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo, vijana wanapaswa kushika hatamu katika kufufua mijadala ya kitaifa inayohusu mustakabali wa maendeleo, kama ilivyokuwa katika misingi ya ujenzi wa taifa tangu uhuru.

“Katika miaka 25 ijayo lazima turudishe mijadala ya maendeleo katika nchi yetu ijadiliwe na vijana na wajipange vyema katika utekelezaji wake kama ilivyokuwa misingi yetu kabla,” aliongeza.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo serikali inazindua dira mpya inayolenga kuongoza maendeleo ya Taifa hadi mwaka 2050, ikijikita katika uchumi jumuishi na shindani, ushiriki mpana wa sekta binafsi, uwezeshaji wa wanawake na vijana, pamoja na mageuzi ya kisera na kijamii.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Mipango, asilimia 81 ya waliotoa maoni kuhusu Dira ya 2050 ni vijana wa kati ya umri wa miaka 15 hadi 35, ishara kuwa kundi hilo lina hamasa kubwa endapo litahamasishwa na kushirikishwa kikamilifu.
Rais Samia amesisitiza kuwa kazi ya maendeleo si ya serikali peke yake, bali ni jukumu la kila Mtanzania – hasa vijana – kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kwa kasi, umoja, na mshikamano wa kizalendo.