×

Ndoa na Shetani – 20

ILIPOISHIA:

“Kwani mwenyeji wangu sijui anaitwa Papaa yupo wapi?”

“Ametoka ghafla.”

“Sasa ametokaje bila kuniachia pesa yangu,” nilikuwa mkali kidogo.

“Dada pesa si tatizo, sema ametoka ghafla ila kaacha maagizo.”

“Maagizo gani?”

“Kuna dereva atakufuata na kukupeleka kwako.”

SASA ENDELEA…

Kwani amekwenda wapi?”

“Dada hiyo siyo juu yangu kujua anakwenda wapi la muhimu kutimiza maelekezo niliyoelekezwa na mkuu.”

“Kwani hapa ni wapi?’

“Dada siwezi kukujibu lolote kwa vile mi si msemaji na nimeagizwa vitu vingine.”

“Kwani muda huu ni saa ngapi?”

“Saa mbili asubuhi.”

“He! Mungu wangu.”

“Kwani vipi?”

“Haiwezekani ataniwekaje mpaka muda huu?”

“Dada mimi sijui lolote.”

“Na kwa nini nibadili nguo kwani zina tatizo gani?”

“Dada humu ndani kuna taratibu zake  nguo hizo huu si muda wake hivyo naomba ufuate maelekezo.”

Nilishangaa akinipa nguo za kitawa nivae, nilijiuliza pale ni wapi na kwa nini nivae nguo za kitawa wakati mimi ni kahaba, tena niliingia katika jumba lile na wenzangu kwa ajili ya biashara ya mwili. Nilijikuta nina maswali mengi ya kumuuliza yule dada aliyeonekana mstaarabu lakini bado nisingeweza kupata majibu ya maana.

Sikutaka kuuliza tena kitu chochote, nilikaa kimya mpaka nione mwisho wake, nilibadili nguo zangu za biashara na kuvaa  nguo za kitawa na rozari yenye msalaba mkubwa kidogo ulikuwa umetulia kifuani. Mmh! Niliamini kumbe mavazi yanaweza kumbadilisha shetani kuonekana malaika.

Baada ya kuvaa vazi lile nilisimama mbele ya kioo na kumuona Konso mwingine kabisa, mwanamke mrembo mcha Mungu aliye tayari kumtumikia Bwana, si yule kahaba aliyefunga safari kuifuata dhambi nchi za watu. Niliamini vazi lile ningesimama nalo mbele ya wazazi wangu wasingepata shida ya kunisamehe kwa vile walikuwa wacha Mungu.

Kwangu lilikuwa fumbo zito kila nilichojiuliza nilikosa jibu na kujiona kama naota kwa kilichotokea muda mfupi kuvua mavazi ya ukahaba na kuvaa mavazi ya kitawa. Nilijiuliza pale nilipo ni sehemu tofauti na jana, lakini hakuna kilichobadilika kwani hata sebule ilikuwa ileile ya jana yake usiku.

Nina imani hata wewe msomaji unashangaa kama mimi kwa kinachoendelea, nilirudisha kumbukumbu uhusiano wa mambo ya muda ule na tukio la jana yake usiku ya kuchukuliwa  na gari mpaka jumba la kifahari mpaka ndani ya jumba lile na kilichoendelea mpaka niliposhtuka asubuhi.

Baada ya kubadili nguo nilipelekwa kwenye chumba cha chakula na kukuta nimeandaliwa  kifungua kinywa kizuri. Baada ya kufungua kinywa nilirudi sebuleni kusubiri dereva aje anichukue. Nilikumbuka mpaka tunalala tulikuwa hatujapatana bei kwa kuamini mteja wangu asingekataa bei yangu.

Nilijiuliza nani atakayenilipa pesa yangu kwa vile maelezo ya dada aliyekuwepo hakueleza kama kaachiwa pesa yangu zaidi ya kusubiri nifuatwe na dereva. Nilikuwa bado nipo njia panda huku nikipepesa macho kuziangalia samani za gharama zilizokuwa pale, yule mdada alisogeza meza ndogo karibu yangu na kuweka glasi kubwa ya lita moja.

Nilijiuliza anataka kuniwekea nini kwenye glasi kubwa kama ile, alikwenda kwenye friji kubwa iliyokuwa karibu na mlango wa kuingia chumba cha chakula na kurudi na bia mbili za Tusker Lite ambazo alikuja kuzifungua na kuzimimina zote kwenye glasi na kunikaribisha.

“Karibu dada.”

“Asante,” niliitikia.

“Wewe endelea mimi naendelea na usafi.”

“Hakuna tatizo.”

Aliondoka na kuelekea upande wa vyumba ilionekana anakwenda kutandika kwenye chumba cha Papaa kama jina lake nilivyolisikia. Sikutaka kujihoji tena kwa vile niliamini ule haukuwa muda wake huenda kina Doi walikuwa wakijua kila kitu juu ya biashara ile.

Kilichonishangaza  shoga zangu kuondoka na kuniacha huku wakijua mimi mgeni japokuwa walinieleza popote nitakapokuwepo siwezi kupotea kurudi nyumbani.

Itaendelea kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment