×

Wakili Ajiondoa Kesi ya Utakatishaji Fedha Inayomkabili Matage na wenzake watano

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha usomwaji wa hoja za awali katika kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi cha dola milioni 4.6 inayomkabili Joseph Matage na wenzake watano, kufuatia wakili anayemtetea mshitakiwa Jamaal Saad kujitoa.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Grace Matage, Jamaal Saad, Mubinkhan Dalwai, Stanley Tibihenda na Edward Omeno na Bushira Ally
kesi hiyo imesikilizwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Gwatwa Mwankuga.
Awali, wakili wa Serikali Neema Kibodya akisaidiana na Pancrasia Protas, amedai kuwa kesi hiyo ililetwa kwa ajili ya kusoma kwa hoja za awali kwa washitakiwa ili iweze kwenda hatua ya usikilizwaji, na kwamba wapo tayari kuendelea.
Kwa upande wake, wakili anayemtetea mshitakiwa Saad, Glori Ulomi amedai kuwa hawapo tayari kuendelea kwa sababu wakili anayemtetea mshitakiwa huyo amejitoa.
“Sisi hatupo tayari kuendelea kwa sababu wakili anayemtetea mshitakiwa namba tatu amejitoa katika shauri hili. Hadi atakapofanya mazungumzo na mshitakiwa huyo ndipo itajulikana kama tuko tayari kuendelea au la,” amedai.
Wakili Neema amedai kuwa wamepokea ombi hilo na hawana pingamizi, ila akaomba Mahakama impe nafasi mshitakiwa Saad aseme kama yupo tayari kuendelea ili kesi iendelee mbele.
Kwa upande wake, Saad ameomba Mahakama impe muda ili aweze kutafuta wakili mwingine.
Hakimu Mwankuga amekubaliana na ombi hilo na kumpa mshitakiwa siku saba kukamilisha hatua hiyo, huku kesi hiyo ikipangwa kuja tena Januari 21, mwaka huu, kwa ajili ya kusomwa kwa hoja hizo.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, ilidaiwa kuwa kati ya Juni mosi na Novemba 30, 2024, wakiwa Dar es Salaam na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washitakiwa wote saba kwa pamoja, kwa nia ovu, walitenda kosa la uhalifu wa kupangwa na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Pia ilidaiwa kuwa kati ya Julai mosi, Agosti 12 na Agosti 26, 2024, ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam,
 washitakiwa wote kwa pamoja walighushi nyaraka za uongo zilizosomwa kama Delivery Order zilizodaiwa kutolewa katika tarehe tajwa, zikionyesha kuwa zilitolewa na kampuni ya Nyota Tanzania Limited, wakala wa Maersk Group, huku wakijua kuwa ni za uongo.
Aidha, ilidaiwa kuwa kati ya Juni mosi na Novemba 30, 2024, ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu, washitakiwa walijipatia mali ambayo ni mafuta ya kupikia aina ya ‘Camar’ yenye uzito wa kilogramu 6,367,262 yenye thamani ya dola 4,627,459.14, mali ya kampuni ya AASTAR TRADING PTE LTD, kwa kudai kuwa malipo ya mali hiyo yalishafanywa na kampuni ya Nyota Tanzania Limited, wakala wa Maersk Group, huku wakijua kuwa ni uongo.
Ilidaiwa zaidi kuwa kati ya Juni mosi na Novemba 30, 2024, washitakiwa walitakatisha fedha kwa kujihusisha na miamala yenye thamani ya dola 4,627,459.14 zilizowekwa katika akaunti yenye jina la ‘Makange Logistics and Traders Company’, huku wakijua kuwa fedha hizo ni mazalia ya kosa la kughushi.

Leave a Comment