
Usajili wa Kilimanjaro International Marathon 2026 unakaribia kufungwa
· Wandaaji wataja tarehe na vituo vya kuchukulia namba za ushiriki.

Ikiwa imesalia karibu mwezi mmoja kabla ya kufanyika mbio za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager (Kili Marathon) kwa mwaka huu wa 2026, ambazo zinasubiriwa kwa hamu kubwa, waandaaji wa mbio hizo wamesema kuwa usajili wa mbio hizo unatarajiwa kufungwa wakati wowote kuanzia sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jijini Dar es Salaam na wanaaji hao, imeonyesha ya kuwa usajili utafungwa mara tu idadi iliyopangwa ya itakapofikiwa dirisha hilo la usajili litafungwa ambapo wanaotarajia kushiriki mbio hizo wametakiwa kutumia muda mfupi uliobaki kufanya usajili wao haraka.
Usajili ulianza kufanyika tangu Oktoba, mwaka jana kupitia mtandao wa www.kilimanjaromarathon.com na ule wa MIXX na YAS kupitia simu ya kiganjani.
Taarifa hiyo, imeendelea kusema kuwa kuna idadi maalum ya washiriki kwenye mbio zote zaKilimanjaro Premium Lager 42km, YAS 21 Km Kili Half Marathon na CRDB 5km Fun Run ili kuhakikisha tukio hilo linafuata kanuni Rasmi za shirikisho la riadha duniani kwa ajili ya kudhibiti usalama wa washiriki.
“Mara tu usajili utakapofungwa, hakutakuwa na viingilio zaidi vinavyouzwa,” ilisema taarifa hiyo.
Wandaaji wa mbio hizo wameendelea kusema kuwa kamati husika itahakikisha washiriki wanafurahia muda wao wakati wa mbio hizo kwa kuepuka misongamano wakati wa kukimbia na pia wanapata huduma zote muhimu wakati wa mbio hizo ikiwemo huduma ya kwanza pale itakapohitajika.
Aidha wandaaji wa mbio hizo wamewakumbusha washiriki kuhakikisha wanachukua namba zao za ushiriki mapema kwenye vituo rasmi za kuchukulia nambari hizo.
Taarifa hiyo imetaja maeneo ya kuchukulia nambari hizo kuwa ni pamoja na Dar es Salaam katika viwanja vya Mlimani City mbele ya Samaki Samaki kuanzia Ijumaa tarehe 13 Machi (saa 10 alasiri-saa moja usiku), Jumamosi tarehe 14 Machi, (saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni).
Eneo la pili litakuwa ni mkoani Arusha katika Hoteli ya Kibo Palace mnamo Jumanne tarehe 17 Machi (saa 8 mchana hadi saa 1 jioni) na Jumatano tarehe 18 Machi, kuanzia saa 8 mchana hadi saa 1 jioni.
Aidha taarifa hiyo imeelezea kituo cha tatu kuwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) mnamo Alhamisi tarehe Machi 19, kuanzia saa 6 mchana – saa 11 jioni, Ijumaa, Machi 20, kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni na Jumamosi Machi 21, kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 11 jioni.
Wadhamini wa mwaka huu ni pamoja na, Kilimanjaro Premium Lager (mdhamini mkuu kilomita 42 Full Marathon), YAS (21km Kili Half Marathon) naBenki ya CRDB ambao ni wadhamini wa mbio za kujifurahisha za kilomita 5.
Wadhamini wengine ni pamoja na Kilimanjaro Water na kampuni ya uzalishaji sukari ya TPC.
Washiriki wengine kwenye eneo la udhamini ni Pamoja na GardaWorld Security, Toyota Tanzania, Columbia Sportswear, Simba Cement, Harleys Healthcare Solutions, ALAF Limited, Sal Salinero Hotel, Kibo Palace Hotels na Keys Hotels.
Mbio za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager zinatarajiwa kufanyika katika viwanja vya chuo kikuu cha ushirika Moshi (MoCU) Jumapili, Machi 22, 2026,ambapo zimeandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro Marathon Limited na Wild Frontiers ndiyo inayohusika na taratibu zote za usafiri wote wa ndani na Pamoja na maswala ya masoko ya kimataifa yanayohusiana na tukio hilo.