
TIMU ya Kijitonyama Veterans imefanya ziara ya kipekee ya kutembelea Vituo Viwili vya Wenye Uhitaji (Watoto Yatima) sambamba na kutoa misaada mbalimbali.Kituo cha kwanza ambacho Kijitonyama Veterans kilianza kukitembelea ni Aliy Bin Abiy Foundation kilichopo Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.Kijitonyama Veterans walimaliza ziara hiyo ya kutoa msaada Street Children and Orphanage Center kilichopo Bunju nje ya Dar.
Ziara hiyo ililenga kutoa msaada wa kijamii na kuonyesha mshikamano kwa Watoto Yatima pamoja na wanaoishi katika mazingira magumu.
Katika ziara hizo mbili Wanachama wa Kijitonyama Veterans walifika vituoni wakiwa na zawadi mbalimbali ikiwemo Chakula, Nguo na vifaaa vya kufanyia usafi.
Mwanasheria wa Kijitonyama Veterans, John Mbitu alizungumza kwa niaba ya Wanachama ambaye aliwapa moyo Watoto hao kwa maneno ya hamasa, akiwahimiza kutokata tamaa na kuamini kuwa ndoto zao zinaweza kufikiwa.

“Kila mmoja wenu ana uwezo wa kufanikisha malengo yake. Msikate tamaa, endeleeni kusimama imara na kuamini katika ndoto zenu,” alisema Mbitu.
Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Kijamii ya Kijitonyama, Kavula Mizeye alitoa wito kwa Makampuni, Taasisi na Veterans nyingine kutoa misaada kwa wahitaji.
Katika ziara hizo zote mbili, Kijitonyama Veterans chini ya Nahodha wake Wilbert Molandi ilicheza michezo ya kirafiki dhidi ya Chanika Veterans na Bunju Veterans yote wakipata sare ya mabao 2-2.
