Mbunge wa Jimbo la Segerea kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Mhe. Agnesta Kaiza, leo amewaalika Waheshimiwa Madiwani wa jimbo hilo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kutembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ziara hiyo imefanyika kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuongozi bila kujali tofauti za vyama vya siasa, pamoja na kuwapa fursa viongozi hao kujifunza na kushuhudia kwa karibu shughuli za Bunge.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Kaiza alisisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya viongozi katika kuwatumikia wananchi wa Segerea kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wao, madiwani hao walimshukuru Mbunge huyo kwa mwaliko huo, wakieleza kuwa ziara hiyo imeongeza uelewa wao kuhusu mifumo ya kibunge na namna bora ya kushirikiana katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Ziara hiyo imeonekana kuwa hatua muhimu ya kujenga daraja la ushirikiano wa kisiasa na kiutendaji kwa manufaa ya wananchi wa Jimbo la Segerea.