
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limewakamata watu 37 kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya kimtandao, ikiwemo kutoa vitisho na kutumia lugha chafu kupitia majukwaa ya mtandaoni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 27, 2026, watuhumiwa hao walikamatwa Aprili 20, 2026 katika eneo la Ubungo kufuatia operesheni maalum iliyofanyika kwa ushirikiano na wananchi pamoja na wadau wa usalama. Operesheni hiyo inalenga kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyoongezeka katika mitandao ya kijamii na mifumo ya kidijitali.
Polisi wamesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa baadhi ya watuhumiwa ni wafanyakazi wa kampuni zinazotoa huduma za mikopo kwa njia ya mtandao, hali inayozua wasiwasi kuhusu matumizi mabaya ya mifumo hiyo kwa madhumuni yasiyo halali.
Miongoni mwa waliotajwa ni Renatus Mujwahuzi maarufu Migeyo, mkazi wa Mbezi Beach; Odilia Oswin maarufu Ngunga, mkazi wa Goba Njia Nne; pamoja na Theresia Brastius maarufu Kanu, mkazi wa Mtoni Kijichi. Watuhumiwa wengine 34 wanaendelea kushikiliwa huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini ukubwa wa mtandao huo wa uhalifu.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa hao, likisisitiza dhamira yake ya kupambana na uhalifu wa mtandaoni unaoweza kuhatarisha usalama wa jamii na ustawi wa wananchi.
Aidha, wananchi wametakiwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka, na wahusika kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria za nchi.