×

Tume Yafichua: Vijana Walirubuniwa kwa Fedha Kushiriki Maandamano, Milioni 5 Yatajwa – Video

Tume ya uchunguzi iliyoundwa kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imeeleza kuwepo kwa ushahidi unaoonyesha namna baadhi ya vijana walivyodanganywa na kushawishiwa kushiriki maandamano.

Akizungumza leo Aprili 23, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha ripoti ya Tume hiyo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Othman Chande, ametoa mfano wa kijana mmoja wa USA River, Arusha, mwenye umri wa miaka 16.

Kwa mujibu wa maelezo yake, kijana huyo alishawishiwa kushiriki maandamano kwa kupewa kiasi cha shilingi elfu 50, huku akiahidiwa atalipwa hadi shilingi milioni 5 endapo angeendelea kushiriki kikamilifu. Inadaiwa pia alielezwa kuwa atapewa “mchongo” utakaomsaidia kutoka kwenye hali ya umasikini.

Jaji Chande amesema ushahidi huo ni miongoni mwa vielelezo vilivyowasilishwa mbele ya Tume na mashahidi mbalimbali, vinavyoonyesha namna baadhi ya vijana walivyotumika katika mazingira ya kushawishiwa na watu waliokuwa na maslahi nyuma ya pazia.

Tume imeeleza kuwa matukio kama haya yanaonyesha umuhimu wa kulinda vijana dhidi ya upotoshaji na ushawishi usio salama, hususan katika nyakati za mivutano ya kisiasa, ili kuepusha kutumika kwao katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.

Leave a Comment