×

Kafulila Aeleza Siri ya Kudumu kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila ameutaja udugu na utamaduni kuwa ni sehemu ya msingi imara wa kudumu kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiwa ni miaka 62 tangu kuwepo kwa muungano huo.

Kafulila ameeleza hilo kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa X ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaoadhimishwa rasmi leo April 26 2026.

Kafulia alitolea mifano ya miungano mingine barani Afrika iliyovunjika ndani ya muda mfupi, ikiwemo ule wa Ethiopia na Eritrea (1952-1962), Ghana-Guinea-Mali (1958-1963), na Senegambia (1982-1989).

Siri ya Mafanikio: Udugu na Utamaduni
Kafulila alieleza kuwa tofauti na miungano mingi ya Ulaya kama Umoja wa Ulaya au ya Asia ambayo inategemea zaidi makubaliano ya kiuchumi na kibiashara, Muungano wa Tanzania ulijengwa juu ya misingi imara ya udugu wa damu, lugha ya Kiswahili, na historia ya pamoja ya kijamii.

Jambo hilo, alisema, linaoufanya Muungano wa Tanzania kuwa na umoja wa watu zaidi kuliko umoja wa serikali pekee.

Alimalizia ujumbe wake kwa kusema: Tutazidi kuwakumbuka Nyerere na Karume siku zote kama hii.

Ujumbe huo umechapishwa ikiwa ni siku ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa Aprili 26, 1964.

Leave a Comment