
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Rwanda unaendelea kuimarika kwa kasi, huku thamani ya biashara kati ya mataifa hayo mawili ikifikia Shilingi bilioni 644 katika mwaka uliopita.
Rais Samia alitoa kauli hiyo Jumapili, Mei 3, 2026, jijini Dar es Salaam baada ya kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, aliyeko nchini kwa ziara ya kikazi.

Mazungumzo hayo yalihusisha pia mawaziri na maofisa waandamizi kutoka pande zote mbili, yakilenga kuimarisha zaidi ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji kwa manufaa ya uchumi wa nchi hizo.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano huo wa kihistoria, akieleza kuwa una mchango mkubwa katika kufungua fursa za ajira, kukuza biashara na kuleta maendeleo ya pamoja kwa wananchi wa Tanzania na Rwanda.
Kwa mujibu wa Rais Samia, kuanzia Machi 1997 hadi Machi 2026, Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania imesajili jumla ya miradi 42 ya uwekezaji kutoka Rwanda yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 325.5.

Aliongeza kuwa miradi hiyo imechangia katika utoaji wa ajira kwa Watanzania 225, hatua aliyoitaja kuwa ni muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi.
Ziara ya Rais Kagame nchini Tanzania inatarajiwa kuendelea kuimarisha zaidi mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizi mbili jirani, huku matarajio yakiwa ni kuongeza kasi ya ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.



