
Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, amewasili nchini Tanzania leo Mei 4, 2026 kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili inayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili jirani.
Rais Ruto anatarajiwa kupokelewa kwa gwaride la heshima na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ya Tanzania jijini Dar es Salaam. Viongozi hao wawili pia watafanya mazungumzo ya uwili yatakayolenga kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, miundombinu na diplomasia ya kikanda.

Kwa mujibu wa ratiba, mapema Mei 5, 2026, Rais Ruto anatarajiwa kuelekea jijini Dodoma ambapo atalihutubia Bunge la Tanzania kabla ya kuhitimisha rasmi ziara yake ya kitaifa.
Ziara hiyo inaonekana kuwa na umuhimu mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Kenya, ambazo ni nchi muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.


