
Tarehe 5 Mei 2026, Airtel Tanzania na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wameingia makubaliano ya kimkakati ya miaka mitatu ya kuimarisha na kupanua jukwaa la mafunzo ya ufundi linalotegemea simu za mkononi, likilenga kuongeza upatikanaji wa elimu ya ujuzi kwa Watanzania kote nchini.
Makubaliano hayo yanaifanya Airtel VSOMO kuwa jukwaa rasmi la taifa la mafunzo ya ufundi stadi mtandaoni chini ya VETA.
Chini ya ushirikiano huo mpya, Airtel Tanzania itaendelea kutoa msaada wa kina kupitia miundombinu ya mawasiliano ya nchi nzima, teknolojia ya kidigitali, huduma ya matumizi bila gharama ya data (zero-rated access), pamoja na kampeni za uhamasishaji zinazolenga kuongeza kasi ya matumizi ya elimu ya kidigitali nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya Airtel katika kuendeleza mageuzi jumuishi ya kidigitali na kupanua upatikanaji wa elimu ya ujuzi kwa Watanzania.
“Airtel VSOMO ni jukwaa rasmi la taifa la mafunzo ya ufundi stadi mtandaoni chini ya VETA. Linawawezesha Watanzania kupata ujuzi wa vitendo wakati wowote na mahali popote kupitia vifaa vyao vya kidigitali,” alisema Kamoto.

Alisisitiza kuwa mchango wa Airtel hauishii kwenye mawasiliano pekee, bali unajumuisha uwekezaji mpana katika ujumuishaji wa kidigitali, elimu na uwezeshaji wa vijana.
“Sisi Airtel hatujihusishi tu na kutoa huduma ya mtandao. Tunahamasisha kikamilifu matumizi ya Airtel VSOMO, tunatoa huduma ya bila gharama ya data, na kuhakikisha gharama si kikwazo kwa Watanzania kujifunza na kujiendeleza,” aliongeza.
Kamoto alibainisha kuwa mfumo wa kidigitali wa Airtel unaendelea kuendesha jukwaa hilo kupitia mtandao mpana wa nchi nzima, huduma imara za data na miundombinu ya fedha kupitia simu, inayowezesha watumiaji kujisajili, kulipia kozi na kupata maudhui ya mafunzo kwa urahisi.
Aliongeza kuwa Airtel ina zaidi ya wateja milioni 23.7 wanaotumia huduma zake, akisema mtandao huo unaiwezesha Airtel VSOMO kuwafikia wanafunzi mijini na vijijini. Pia alieleza kuwa huduma ya matumizi ya bure ya data imepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za elimu ya mtandaoni kwa maelfu ya watumiaji.
Takwimu za Airtel zinaonesha kuwa Airtel VSOMO imepakuliwa mara 59,000, ambapo takribani asilimia 60 ya matumizi yamefanyika kupitia huduma ya bure ya data ya Airtel. Jumla ya watumiaji 27,194 wamejisajili kwenye jukwaa hilo, huku wanafunzi 9,539 wakijiunga na programu mbalimbali za ufundi stadi.
Kati ya hao, wanafunzi 6,723 tayari wamehitimu mafunzo yao, jambo linaloonesha ongezeko la matumizi na mafanikio katika elimu ya ufundi stadi ya kidigitali.
Airtel pia imewekeza tena takribani TZS milioni 80.6 kutoka katika sehemu ya ada za mafunzo kurudi VETA ili kusaidia upanuzi wa jukwaa, uandaaji wa maudhui na uimarishaji wa mifumo. Aidha, Airtel VSOMO imezalisha thamani ya kiuchumi inayokadiriwa kufikia TZS bilioni 1.2, huku wanafunzi wakihifadhi wastani wa TZS 180,000 kila mmoja ikilinganishwa na njia za kawaida za mafunzo.
Jukwaa la Airtel VSOMO pia limeunganishwa na mfumo wa Fundi Connect, unaowawezesha wahitimu wa VETA kusajili ujuzi wao na kuunganishwa moja kwa moja na wateja, hivyo kuimarisha uhusiano kati ya mafunzo na ajira pamoja na kusaidia ujasiriamali wa vijana.
Airtel VSOMO pia inalingana na mradi wa East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP), unaolenga kutambua na kusawazisha vyeti vya ufundi stadi kati ya Tanzania, Kenya na Ethiopia, hatua inayoongeza uhamaji wa wafanyakazi na fursa za ajira kikanda.
Ushirikiano huo unaunga mkono ajenda ya maendeleo ya taifa chini ya Dira ya Maendeleo 2030, na kuimarisha juhudi za serikali za kuongeza ajira kwa vijana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA alitoa shukrani kwa Airtel Tanzania kwa kuendelea kusaidia maendeleo ya elimu ya ufundi kupitia mageuzi ya kidigitali.
“Tunaishukuru sana Airtel Tanzania kwa msaada wao endelevu, hasa katika kutoa huduma ya intaneti na kuwezesha upatikanaji mpana wa Airtel VSOMO. Ushirikiano huu umetuwezesha kuwafikia vijana wengi zaidi kuliko hapo awali,” alisema.
Alibainisha kuwa ushirikiano huo umeongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mafunzo na kuboresha unyumbufu wa utoaji wa elimu nchini.
Aliongeza kuwa Airtel VSOMO sasa ni mfumo rasmi wa kidigitali wa mafunzo ya ufundi stadi chini ya VETA, unaokamilisha vituo vya mafunzo vya kawaida na kupanua wigo wa kitaifa.
Pia alieleza kuwa awali VETA ilikuwa inapokea maombi takribani 12,000 kwa mwaka, lakini uwezo wake ulikuwa unaruhusu kuchukua wanafunzi 3,000 pekee kutokana na vikwazo vya miundombinu ya vituo vya mafunzo.
“Kupitia Airtel VSOMO, tunapanua wigo ili vijana wengi zaidi wapate ujuzi wa vitendo kwa ajili ya ajira na kujiajiri popote walipo,” alisema.
Taasisizo hizo mbili zimeweka lengo la pamoja la kuandikisha angalau wanafunzi 400 wapya kila mwezi kupitia Airtel VSOMO, kama sehemu ya kuendelea kupanua elimu ya ujuzi wa kidigitali na kuimarisha ajira kwa vijana nchini Tanzania.