
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kusitisha operesheni ya kijeshi ya Marekani ya kusindikiza meli katika Mlango Bahari wa Hormuz, operesheni iliyojulikana kama “Project Freedom,” baada ya kutekelezwa kwa muda mfupi wa siku moja.
Trump amesema hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Marekani na Iran, kwa lengo la kupunguza na hatimaye kumaliza mivutano inayoendelea Mashariki ya Kati.
Mlango Bahari wa Hormuz, ambao ni njia muhimu sana ya usafirishaji wa mafuta duniani, umeendelea kuwa eneo lenye mvutano mkubwa kutokana na migogoro ya kisiasa na kiusalama kati ya mataifa hayo mawili. Kusitishwa kwa operesheni hiyo kunatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Washington kupunguza presha ya kijeshi huku ikisukuma diplomasia mbele.

Hatua hiyo imekuja wakati dunia ikiendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama katika eneo hilo, ambapo mataifa mbalimbali yameonyesha wasiwasi juu ya athari za kiuchumi na kiusalama endapo hali ya mvutano itaendelea kuongezeka.
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema kuwa Marekani imekamilisha baadhi ya shughuli zake za kijeshi dhidi ya Iran, lakini imeonya kuwa bado iko tayari kujibu kwa nguvu endapo kutatokea mashambulizi yoyote dhidi ya meli zinazopita katika eneo hilo la kimkakati.
Kwa sasa, macho ya dunia yanaelekezwa katika hatua za kidiplomasia, huku kukiwa na matumaini kwamba mazungumzo yanaweza kupunguza kasi ya mzozo huo unaotishia usalama wa kimataifa.