
RAIS Samia leo Septemba 29, 2022 amesema mawakili wa Serikali ni ‘jeshi kubwa’ linalotakiwa kulinda uchumi wa Tanzania kwa kutumiia kalamu zao.
Pia, amesema kuanzia sasa ni marufuku kusainiwa mikataba ya Serikali bila kushirikisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Huko nyuma mikataba ilisainiwa bila ofisi ya AG kufahamu na wanapopata tatizo ndio wanaikumbuka ofisi hiyo huku waliosani wamestaafu au wametangulia mbele ya haki.
Rais Samia amesema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa kuanzishwa chama cha kitaaluma cha mawakili wa Serikali jijini Dodona.

“Nyinyi ndio ‘majeshi wa kulinda uchumi wetu, kisheria uchumi wetu lazima ulindwe, uwekezaji lazima ulindwe, biashara lazima zilindwe na walinzi wa hayo ni nyinyi.
“Nyinyi ni walinzi wa kalamu na siyo walinzi wa mabunduki. Ni walinzi wa kalamu na sheria zenu. Kwa hiyo mwende mkalinde uchumi wetu, kihaki kabisa kiuadilifu kabisa ili nchi hii, iweze kupokea wawekezaji wengi zaidi, tuwekeze zaidi, tukuze uchumi masilahi yapatikane,” amesema Rais Samia.

“Tukilinda uwekezaji unaowekezwa Tanzania tutakwenda kupanua wigo mpana unaokuza uchumi, wigo mpana wa kukusanya mapato na yale mliolalamikia hapa itakuwa rahisi Serikali kuyatimiza kwenu,” amsema Rais Samia huku akihaidi atawapa fungu waliloomba ili kulinda uwekezaji na kukuza uchumi.
Pia, Rais Samia amewataka mawakili wa Serikali ambao hawajajisajili kwenye daftari la mawakili wa Serikali wakafanye hivyo wakati bado muda upo.

“Nirudie kwa ambao bado hawajajisajili, basi wahimize wajisajili, vinginevyo baada ya muda kupita hatutawatambua kama ni mawakili wa Serikali.
“Itabidi ama watafute sekta nje waingine, ama sijui watapewa msamaha gani na Mwanasheria Mkuu ili waingie tena kama mawakili wa Serikali.

Hadi sasa kwa mujibu wa Rais Samia mawakili wa Serikali ni 2,652 na kuna wengine bado hawajajisajili kwenye daftarri hilo ambalo liko kwa mujibu wa sheria.
Pia, Rais Samia alisema amefurahishwa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Dk Eliezer Feleshi kwamba chama hicho kipya kitashirikiana na Chama cha Mawakili Tanganyika, (Tanganyika Law Society-TLS) kwa kufanya kazi pamoja.