
Mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya gari aina ya Actros Benz lenye namba za usajili SSD 319 AB / SSD 953 AB kupinduka na kisha kuwaka moto katika kijiji cha Rukindo, kata ya Katoma, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi Blasius Chatanda, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa ajali ilitokea Mei 10, 2026 majira ya saa nane mchana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gari hilo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Sudan Kusini kabla ya kupinduka baada ya dereva kushindwa kulimudu kwenye mteremko mkali.

Ajali hiyo ilisababisha kifo cha dereva, Shafii Mohamod Omary mwenye umri wa miaka 27, mkazi wa Kenya, huku abiria mwingine, Tingo Nelson Kprimo (28), akijeruhiwa.
Polisi wamesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kuchukua tahadhari barabarani katika eneo lenye mteremko mkali, hali iliyosababisha gari kupoteza mwelekeo na baadaye kuwaka moto.
Majeruhi amepelekwa hospitali kwa matibabu huku uchunguzi zaidi ukiendelea kubaini ukubwa wa hasara iliyosababishwa na ajali hiyo.







STORI NA DENIS RUTA, GPL – KAGERA