
Simanzi imetanda katika familia ya mfanyabiashara Sifaeli Mollel baada ya mwili wake kukutwa ukiwa umeharibika ndani ya nyumba inayodaiwa kutumiwa na mganga wa jadi, iliyopo eneo la Muriet, jijini Arusha.
Mollel (48), mkazi wa Kijenge katika Kata ya Kimandolu, aliripotiwa kutoweka Mei 3, 2026 katika mazingira ya kutatanisha, kabla ya mwili wake kugundulika siku saba baadaye, tukio lililozua hofu na mshangao mkubwa kwa familia yake pamoja na wakazi wa eneo hilo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kupitia Kamanda wake Justine Masejo limethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na kusema linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kifo hicho pamoja na watu wote wanaoweza kuhusika, huku likiahidi kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuhusika.
Ndugu wa marehemu wamesema mazingira ya tukio hilo yameacha maswali mengi, wakidai kuwepo kwa viashiria vinavyoweza kuhusisha uhalifu, ikiwemo vitu vya tiba asili pamoja na vitambulisho vyenye majina tofauti vilivyokutwa ndani ya nyumba hiyo. Wameiomba polisi kuongeza kasi ya uchunguzi ili kubaini ukweli wa kilichotokea.