
Mjadala wa makubaliano kati ya Marekani na Iran umeingia katika hatua mpya ya mvutano baada ya Tehran kusema haitakubali mkataba wowote ambao hautalinda kikamilifu haki za taifa hilo.
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, amesema serikali ya Iran haitaidhinisha makubaliano yoyote hadi ihakikishe kuwa maslahi ya wananchi wake yamezingatiwa kikamilifu.
Kauli hiyo imekuja baada ya ripoti kutoka vyombo vya habari vya Marekani kudai kuwa Rais Donald Trump ametuma mfumo mpya wa makubaliano wenye masharti magumu zaidi kwa Iran.
Trump amesema moja ya vipaumbele vyake vikubwa ni kuhakikisha Iran haitengenezi silaha za nyuklia pamoja na kufunguliwa tena kwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta ya Hormuz.
Katika mahojiano na Fox News, Trump alisema hana haraka ya kufikia makubaliano na akaonya kuwa Marekani inaweza kuchukua hatua nyingine za kijeshi ikiwa haitapata kile inachokitaka.
Kwa upande wake, Iran imesisitiza kuwa lazima ipate dola bilioni 12 kuzuiwa nje ya nchi kabla ya kuanza mazungumzo ya kina kuhusu mpango wake wa nyuklia. Iran pia imekanusha madai ya Trump kuwa akiba yake ya uranium iliyoimarishwa ingeangamizwa chini ya makubaliano hayo.
Wakati diplomasia ikiendelea, hali ya usalama bado ni tete baada ya mapigano ya hapa na pale kuendelea licha ya makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Aprili.
Vyombo vya habari vya Iran vimedai kuwa Walinzi wa Mapinduzi walidungua ndege ya kijeshi isiyo na rubani ya Marekani iliyokuwa karibu kuingia katika anga ya Iran, ingawa Washington bado haijathibitisha taarifa hiyo.
Mvutano huo umeongeza hofu kuhusu usalama wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta ya dunia. Iran pia imeashiria mpango mpya wa kuimarisha mamlaka yake katika eneo hilo kupitia hatua za bunge.