
Kuna watu hujikuta wakiwa na homa na kudai wana malaria kumbe ni ugonjwa wa UTI. Tunawalete tofauti za magonjwa hayo.
UTI ni maambukizi kwenye njia ya mkojo na Malaria ni homa itokanayo na maambukizi baada ya kuumwa na mbu, haya ni magonjwa mawili tofauti yanayohitaji matibabu sahihi. Hapa kuna tofauti zake kuu kwa ufupi:
1. Chanzo cha Ugonjwa
Malaria: Husababishwa na vimelea aina ya Plasmodium vinavyoingia mwilini kupitia kuumwa na mbu jike mwenye vimelea viitwavyo Anopheles. Dalili kuu za malaria ni pamoja na homa kali, kutetemeka kwa baridi, na kutoka jasho jingi. Dalili hizi kawaida huanza kujitokeza siku 10 hadi 15 baada ya kuumwa na mbu aliyeambukizwa.
Dalili hizo mara nyingi huambatana na yafuatayo: Maumivu ya kichwa, kichefuchefu na kutapika, maumivu ya misuli na viungo, pamoja na uchovu mwingi.Dalili kwa watoto Kukosa hamu ya kula, kuhara, au kuonekana mwenye udhaifu mkubwa.

UTI: Ni tofauti na malaria kama nilivyoeleza hapo juu. UTI husababishwa na bakteria (kama E. coli) wanaoanzia kwenye mfumo wa utumbo na kuingia kwenye njia ya mkojo (kibofu au figo). Ikiwa maambukizi hayatotibiwa, yanaweza kuendelea kuenea, na hatimaye kufikia figo kama kiungo muhimu cha mwili kilichopo katika sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo (upper urinary tract).
2. Dalili Kuu
Dalili za Malaria: Homa kali, baridi na kutetemeka, maumivu ya kichwa, maumivu ya viungo na misuli, na kichefuchefu.
Dalili za UTI: Maambukizi ya UTI kwa kawaida huwapata zaidi wanawake, ingawa wanaume wanaweza pia kupata.
Dalili za UTI zinaweza kujumuisha maumivu wakati wa kukojoa na kukojoa mara kwa mara, mkojo wenye harufu isiyo ya kawaida, mkojo uliochanganyika na damu, na maumivu katika sehemu ya chini ya tumbo.
Dalili ya homa, kichefuchefu, na maumivu katika sehemu ya juu ya tumbo inaweza kuwa ni ishara kwamba maambukizi husika yamefikia sehemu za juu za mfumo wa mkojo. Sehemu hizi hujumuisha figo pamoja na ureta, yaani mirija inayosafirisha mkojo kutoka kwenye kibofu kwenda nje ya mwili.
3. Utambuzi na Matibabu
Vipimo: Malaria hugunduliwa kwa kipimo cha damu, wakati UTI hugunduliwa kwa kipimo cha mkojo (Urinalysis/Urine Culture).
Dawa: Malaria hutibiwa kwa dawa za kuzuia malaria (kama ACTs), huku UTI ikitibiwa kwa dawa za kuua bakteria (Antibiotics).
Kumbuka: Mgonjwa anaweza kupata magonjwa yote mawili kwa pamoja, hivyo ni muhimu kupima damu na mkojo hospitalini badala ya kujitibia kwa mazoea.
Stori na Elvan Stambuli, Global Digital