
Mvutano kati ya Iran na Marekani umeongezeka kwa kasi baada ya Iran kudai kuhusika na mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Marekani katika nchi za Kuwait na Bahrain, ikiwa ni pamoja na makao makuu ya Kikosi cha Tano cha Jeshi la Wanamaji la Marekani (US Fifth Fleet).
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) limesema lilirusha makombora na droni kulenga kambi za kijeshi na helikopta katika nchi moja ya Ghuba, likidai ni majibu ya shambulio la Marekani dhidi ya mnara wa mawasiliano kusini mwa Kisiwa cha Qeshm.
Kwa upande wake, mamlaka za kijeshi za Kuwait zimeripoti kuwa jengo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kuwait limepata uharibifu mkubwa kutokana na kile kilichoelezwa kama shambulio la Iran, huku watu kadhaa wakiripotiwa kujeruhiwa na kupata matibabu.
Mamlaka ya usafiri wa anga Kuwait pia ilithibitisha kusitishwa kwa safari za ndege kwa muda na ndege kuelekezwa viwanja vingine vya ndege kutokana na hali ya usalama.
Bahrain nayo iliwasha ving’ora vya tahadhari na kuwataka wananchi kujikinga baada ya taarifa za mashambulizi ya makombora na droni katika eneo hilo.
Iran, kupitia vyombo vyake vya habari, pia iliripoti kuwa IRGC ililenga meli moja inayoitwa Panaya, ikidai ilikuwa ni hatua ya kulipiza kisasi baada ya Marekani kushambulia meli ya mafuta ya Iran karibu na Mlango wa Hormuz.
Jeshi la Marekani kupitia Central Command (CENTCOM) limetupilia mbali baadhi ya madai ya Iran, likisema liliweza kuzuia mashambulizi ya makombora na droni yaliyolenga washirika wake katika Ghuba, na kulenga maeneo ya Iran kama sehemu ya majibu yake.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha taarifa za kusitishwa kwa mazungumzo kati ya Washington na Tehran, akisisitiza kuwa mawasiliano bado yanaendelea licha ya hali ya mivutano.
Mvutano huo umeathiri pia biashara ya kimataifa, ambapo usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz njia muhimu ya mafuta duniani umesemekana kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana na hali ya usalama isiyotabirika.
Shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF limeonya kuwa mgogoro huo unaathiri pia usambazaji wa misaada ya kibinadamu katika maeneo mbalimbali duniani kutokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji na misukosuko ya ugavi.
Hadi sasa, hali bado ni tete huku dunia ikihofia kuongezeka zaidi kwa mgogoro huo unaoendelea kusambaa katika eneo la Mashariki ya Kati.